Prisons yaigomea Simba, Kaburu auteka Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

Kaburu na aliyekuwa rais wa Simba, Evans Aveva waliachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea shtaka la utakatishaji wa fedha, lililowafanya kukaa ndani kwa zaidi ya miaka miwili.

Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC imelazimishwa suluhu na Tanzania Prisons mbele ya makamu wake wa rais wa zamani Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanaifanya Prisons kufuta uteja wake wa miaka tisa tangu mwaka 2009 imekuwa ikipokea vipigo mfululizo kila inapokutana na Simba jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo leo hali imekuwa tofauti kwani nidhamu ya uchezaji hasa katika kukaba imeibeba timu hiyo kwa kiasi kikubwa mbele ya Simba.

Prisons walikaba wote na kushambulia wote kila walipokuwa na mpira hivyo kuifanya Simba kupata wakati mgumu kuipenya ngome yao.

Beki wa Prisons, Nurdin Chona alimficha mshambiliaji msumbufu Meddie Kagere na kusababisha asifurukute kabisa katika mchezo wa leo.

Pia licha ya kufuta uteja pia Prisons imeendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza mchezo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Prisons inayonolewa na kocha Mohammed Rishard 'Adolph' ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo mpaka Sasa kwenye Ligi Kuu Bara.

Simba ilianza kwa kasi mchezo huo, lakini ilikutana na uimara was wachezaji was Prisons ambao walikuwa na nidhamu ya ukabaji.

Wachezaji was Prisons wameonekana wako fiti na wanakaba kwa nidhamu hivyo kuwapa wakati mgumu washambuliaji was Simba wakiongozwa na Meddie Kagere kupata mabao.

Licha ya viunho Jonas Mkude na Ibrahin Ajib kutoa pasi za kipenyeza kwa Kagere na Kahata dakika ya 20, 26 na 35 lakini pass hizo zilinaswa na wachezaji wa Prisons.

Nusura Simba ifungwe dakika ya 30 baada ya Benjamin Asukile kuambaa na mpira kutoka katikati ya Uwanja na wakati akijiandaa kupiga alivaana na kipa Aishi Manula hivyo wote kuanguka chini na mpira huo kiwapita na kutoka nje.

Simba walijibu mapigo dakika ya 44 kwa kufanya shambulizi Kali lililowapa faulo ambayo hata hivyo Ajib alipiga faulo hiyo ba kupasha.

Dakika 10 za mwisho za kipindi cha Kwanza ziligeuka kuwa za ubabe hivyo kupelekea wachezaji kufanyiana madhambi na kuumizana wakati wakiwania mpira.

Shomari Kapombe alijikuta akiugukia maumivu baada ya kufanyiwa madhambi na vedastus Mwihambi huku pia Benjamin Asukile nae alitolewa nje kwa machela baada ya kufanyiwa madhambi na Ibrahim Ajib.

Kaburu atinga Uwanja wa Uhuru

Saa 48, baada ya kuachiwa kwa dhamana Makamu wa rais wa zamani wa Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ ameibukia Uwanja wa Uhuru na kuishuhudia Simba ikilazimishwa suluhu na Tanzania Prisons.

Kaburu mmoja wa wapenzi wa kubwa wa soka ikiwa ni siku yake ya tatu akiwa nje baada ya kupata dhamana alionekana jukwaani uwanja wa Uhuru kushuhudia timu yake ya Simba.

Kaburu aliingia uwanjani hapo mpira ukiwa tayari umeanza na kwenda kukaa jukwaa kuu upande ambao mara nyingi hukaa mashabiki wa Simba.

Wakati anakwenda kukaa jukwaani alisalimiana na watu mbalimbali akiwemo mashabiki na mwanachama wa Simba na kuiibua shangwe.

Kaburu na aliyekuwa rais wa Simba, Evans Aveva waliachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea shtaka la utakatishaji wa fedha, lililowafanya kukaa ndani kwa zaidi ya miaka miwili.