Tanzania yanusa medali nyingine Tenisi Afrika

Muktasari:

Mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi nane yanafikia tamati leo huku mabingwa wakipata nafasi ya kuiwakilisha Afrika Mashariki na Kati kwenye mashindano ya Afrika ya Vijana baadae Machi nchini Togo na Madagascar.

Dar es Salaam.Tanzania imejiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa medali nyingine ya shaba katika mashindano ya Tenisi Afrika Mashariki na Kati yanayofikia tamati leo kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Tanzania inahitaji ushindi katika mechi moja kati ya mbili zilizosalia ili kujihakikishia medali hiyo katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Shelisheli.

Isaka Ndossi ameitanguliza Tanzania katika nafasi ya kutwaa medali hiyo baada ya kumfunga Rona Tuyishine wa Shelisheli kwa seti 2-0 za 6-3 na 6-2.

Tanzania sasa inahitaji kushinda mchezo wa pili ili kujihakikishia medali ya shaba hata kama itafungwa mechi ya tatu ya doubles.

Rashid Ramadhan atamkabiri Matteo Lavigne wa Shelisheli katika mchezo wa pili ambao kama atashinda, Tanzania itajihakikishia medali ya shaba hata kama itafungwa kwenye mchezo wa tatu wa Doubles.

Awali, Timu ya wasichana chini ya miaka 16 iliipatia medali ya shaba huku Kenya ikitwaa ubingwa.

Kenya imetawazwa kuwa bingwa mpya kwa kuichapa Uganda katika michezo miwili kati ya mitatu ya fainali.

Alicia Owegi amemfunga Shanita Namagembe kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0 wakati Angela Akutonyi akimchapa Winnie Birungi kwa seti 2-0 za 6-1 na 6-2.

Kwa wasichana chini ya miaka 14, Tanzania itacheza na Uganda baadae jioni kutafuta mshindi wa tatu huku Kenya ikicheza fainali na Rwanda.

Huku kwa wavulana chini ya miaka 16, Tanzania itasaka mshindi wa tatu dhidi ya Kenya wakati Uganda ikicheza Burundi fainali.