Kikosi cha ‘mapro’ wa Kitanzania wanaotesa nje

Monday December 9 2019

Mwanaspoti-Samatta-Msuva-Kikosi-mapro-Kitanzania-wanaotesa-nje-Soka-Tanzania

 

By Eliya Solomon

Ubabe wa mataifa kama vile Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Misri, Tunisia na Algeria kwenye soka la Afrika, umechangiwa  na idadi kubwa  ya wachezaji wao ambao wanacheza soka la kulipwa kwenye Ligi zenye ushindani wa juu.
Kuthubutu kwa Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kwa kiasi kikubwa kumekuwa chachu ya wachezaji wengine wa Kitanzania kuingiwa na shauku ya kutaka kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.
Samatta alianza kuonyesha 2011, kuna inawezekana kimataifa  mara baada ya kutua TP Mazembe ambako alikutana na Mtanzania mwenzake, Thomas Ulimwengu aliyetokea kwenye akademi ya AFC Eskilstuna, iitwayo Athletic FC.
Wapo wachezaji wengi wa Kitanzania ambao walifuata nyayo za Samatta. Hiki ni kikosi cha nyota  11 wa Kitanzania wanaotesa kwenye ligi za ushindani ndani na nje ya Afrika.

1. David Kissu  (Gor Mahia/ Kenya)
Licha ya kuwa huu ni msimu wake wa kwanza katika klabu ya Gor Mahia amekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho huku akimweka benchi Boniface Oluoch ambaye alikuwa akitegemewa na  mabingwa hao watetezi wa  Ligi Kuu Kenya.
Akiwa nchini Tanzania, Kissu  ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa  Kilimanjaro Stars walipo Uganda kwa mashindano ya Cecafa Chalenji, alizichezea Njombe Mji, Toto Africans ya Mwanza na Singida United kabla ya kutimkia zake Kenya.
Kipa huyo alijichotea umaarufu nchini Kenya baada ya kucheza mkwaju wa penalti katika mechi ya kuwania nafasi ya kuingia makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya DC Motema Pembe, Oktoba 27 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

2. Hassan Kessy  (Nkana/Zambia)
Beki wa kulia wa zamani wa Yanga na Simba, Hassan Kessy amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi chake cha Nkana ambayo iliondolewa na Simba kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Kuondolewa kwao na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa kulimfanya Kessy na Nkana yake kuhamia Kombe la Shirikisho ambalo walipata nafasi ya kuingia makundi.
Tangu ajiunge na Nkana, Agosti 3 mwaka jana amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na ameisaidia timu hiyo ndani ya msimu wake wa kwanza kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Zambia ‘MTN/FAZ’ na pia kuchukua ubingwa wa kombe la Barclays.

3. Jamal  Mwambeleko  (KCB/ Kenya)
Mwambeleko na Manyika walinaswa kwa pamoja na KCB mara baada ya kuvunja mikataba yao, beki huyo wa kushoto mwenye uwezo pia wa kucheza winga amekuwa miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo ambao wanaunda safu ya ulinzi.
4. Abdi  Banda  (Highlands/Afrika Kusini)
Banda amerejea kwenye ufiti wake baada ya kupona majeraha, yaliyokuwa yalimsumbua  kiasi cha  kushindwa msimu uliopita kuachwa na klabu aliyokuwa akiichezea  ya  Baroka.
Baada ya kuachwa na klabu hiyo, Banda ameibukia Highlands Park F.C. na tayari ameingia katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo na yenyewe inashiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

5. Aman  Kyatta  (Kariobangi/ Kenya)
Mchaga Aman Kyata ambaye ni beki wa kati wa F.C. Kariobangi Sharks  yupo kwenye kiwango bora zaidi kwa sasa, mbali na kuzuia ana uwezo pia wa kufunga. Msimu uliopita alipokuwa akiiochezea  Posta Rangers aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa Kitanzania kufunga bao kwenye Ligi Kuu Kenya  ndani ya msimu huo.

6. Abdallah Hamis (Opara United/Botswana)
Abdallah Hamis ni miongoni mwa viungo bora wa Kinzania ambao wanacheza nafasi ya ukabaji (6). Amekuwa na mwanzo mzuri wa  msimu akiwa na Orapa United inayoshiriki Ligi Kuu Botswana.

7. Michael Lema (SK Sturm Graz/ Austria)
Lema ambaye ni mzaliwa wa Itigi mkoani Singida amekuwa kwenye moto wa kuotea mbali kiasi kwamba kocha wa kikosi cha kwanza cha SK Sturm Graz, Roman Mahlich aliamua kuanza kumtumia.
Awali Lema aliuanza msimu uliopita  wa 2018/19 kwa kukichezea kikosi B cha timu hiyo ambacho amekifungia  mabao 13 kwenye michezo 12 ya ligi daraja la pili ambalo ni maarufu kama Regionalliga Mitte.
Kiwango alichikionyesha huko kilimvutia Roman na kuanza kutoa nafasi kwa kinda huyo ambaye kwa  sasa  anakichezea  kikosi cha kwanza cha SK Sturm Graz kinachoshiriki Ligi Kuu Austria.

8. Himid Mao (Enppi/ Misri)
Himid ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi zote za viungo kwa maana ya namba sita na nane, msimu uliopita aliifungia mabao mawili Petrojet ambayo ilishuka daraja. Kwa sasa Himid anaichezea Enppi Sporting Club.

9. Mbwana Samatta (KRC Genk/ Ubelgiji)
Samatta amekuwa katika kiwango bora, msimu huu ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya huku katika mchezo huo akifunga bao.
Aliweka rekodi hiyo, Septemba 17 mwaka huu nchini Austria licha ya kuwa mchezo huo, walipoteza kwa mabao 6-2, alifunga bao lake la kwanza nchini humo hadi sasa mshambuliaji huyo, ana mabao matatu katika mashindano hayo.

10. Saimon Msuva (Difaa/ Morocco)
Ukiwa na Msuva kwenye timu una faida ya kumtumia kwenye maeneo yote ya ushambuliaji.
Nyota huyo wa Difaa El Jadida ya Morocco anauwezo wa kucheza kwenye wingi zote mbili na pia kama namba tisa au 10.
Amekuwa kwenye kiwango bora kwa muda mrefu, hakupata shida kwenye msimu wake wa kwanza kuzoea mazingira ya Morocco na badala yake aliwashangaza wengi kwa kufunga mabao 11 kwenye Ligi ya nchini hiyo ‘Batola Pro’.
Msimu uliofuata Msuva alipachika mabao 13 maana yake ni kwamba alivunja rekodi yake ya msimu wake wa kwanza nchini humo, msimu huu ambao ndio kwanza umeanza tayari katika akaunti yake ya mabao anayomawili.

11. Farid Mussa (Tenerife B/ Hispania)
Licha ya kuwa kikosi B cha Tenerife amekuwa akifanya vizuri katika madaraja ya chini Hispania na kikosi hicho.  Kasi na ubunifu alionao umekuwa ukimsaidia kuwatambuka mabeki mbalimbali ambao amekuwa akikumbana nao.
Hao ni baadhi ya wachezaji wa Kitanzania wanaofanya vizuri kwa sasa licha ya uwepo wa orodha ndefu ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akiwemo Elias Maguli wa Nakambala Leopards, Eliuter Mpepo wa  Buildcon zote za Zambia.

Advertisement