Nonga anakitaka kiatu cha Kagere

Muktasari:

Nonga ambaye ni miongoni mwa wachezaji wasomi Ligi Kuu, aliwahi kupata nafasi ya kuichezea Yanga baada ya kufanya vizuri akiwa na Mwadui licha ya kuwa uwezo wake ulianza kuonekana akizichezea JKT Oljoro

Dar es Salaam. Miongoni mwa washambuliaji wanaoonekana kuwa tishio msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni pamoja na Paul Nonga wa Lipuli  mwenye mabao saba katika orodha ya wafungaji  wa Ligi hiyo maarufu kama VPL.
Msimu huu wa 2019/20 wazawa wameonakana kuja  juu, akiwemo Nonga  kiasi cha kuanza kutishia uwezekano wa mshambulioaji hatari wa Simba, Meddie Kagere kutetea tuzo yake ya ufungaji bora licha ya kuongoza  akiwa na mabao manane.
Nonga ambaye ana uzoefu wa kucheza VPL kwa muda mrefu, anasema siri ya kuwa katika kiwango bora cha ufungaji msimu huu ni kutokana na kuzungukwa na wachezaji wanaojua namna ya kucheza naye katika kikosi cha Lipuli.
“Kufanya vizuri kwa mshambuliaji kunategemea na ushirikiano kutoka kwa wenzake, nimekuwa nikishirikiana vyema na wenzangu kiasi cha kuweza kufunga mara kwa mara. Tuna malengo ya kumaliza katika nafasi za juu hivyo nawajibika kutoa mchango.
“Hayo ni malengo ya timu lakini upande wangu natamani kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu. Inawezekana.  Kikubwa ni kuomba Mungu aendelee kunipa nguvu na kuniepusha na majeraha,” anasema nyota huyo.
Kagere wa Simba, anamtaja kama  miongoni  mwa   washambuliaji wazuri ambao anafurahia uwepo wao katika  Ligi  kwani wamekuwa  chachu kwake ya kujituma zaidi katika vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora.
Nonga ambaye ni miongoni mwa wachezaji wasomi Ligi Kuu, aliwahi kupata nafasi ya kuichezea Yanga baada ya kufanya vizuri akiwa na Mwadui licha ya kuwa uwezo wake ulianza kuonekana akizichezea JKT Oljoro.
Yanga ilimsajili Nonga kipindi ambacho kikosi chao katika idara ya ushambuliaji kilikuwa kimesheheni yota wengine  waliokuwa wakifanya vizuri   kama vile  Mrundi Amis  Tambwe, Donald Ngoma, Malimi Busungu, na Matheo Anthony.
“Ilikuwa rahisi kwangu kujiunga na Yanga kwa sababu walinipa kiasi kikubwa cha fedha, isingekuwa rahisi kukipata nikiwa Mwadui, niliamini naweza kufanya vizuri, ushindani wa namba ulikuwa mkubwa kutokana na aina ya wachezaji ambao nilikumbana nao,” anasema Nonga.
Katika vituko ambavyo  mshambuliaji huyo, alikumbana navyo akiwa Yanga ni pamoja na siku moja kujikuta kichwani amenyolewa nywele kidogo, “Ni kama waliamua kunikaribisha kwa sababu ishu za ushirikina zilikuwa zimeshika kasi.”
Akiizungumzia pia Mbeya City iliyostua Ligi Kuu Tanzania Bara, Nonga ambaye aliichezea timu hiyo, anasema walijivunia ubora wao maana hadi vigogo wa soka nchini walikuwa wakikumbana na vichapo wakicheza nao.
“Siwezi kuisahau Mbeya City, tulikuwa timu hasa lakini kuondoka kwa mchezaji mmoja baada ya mwingine ilichangia kupungua kwa ubora wa timu,” anasema.
Nonga anasema wasichojua wengi kuhusu yeye ni kwamba baba yake alikuwa mtu wa dini sana hivyo alitaka kumuona akifuata uelekeo huo na siku moja awe padri, lakini utundu wake uliyeyusha ndoto hiyo ya mzee wake.
Na sasa amekuwa nyota wa soka.