Mtanzania atwaa medali ya fedha tenisi Afrika

Muktasari:

Tegemeo la medali ya dhahabu kwa Tanzania limesalia kwa Kanuti Alagwa atakayecheza fainali ya vijana chini ya miaka 16 na Junior Mfashingabo wa Rwanda leo jioni.

Dar es Salaam.Mtanzania Rashid Ramadhan ametwaa medali ya fedha katika mashindano ya Tenisi Afrika mashariki na kati ya kanda yanayofungwa leo kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Rashid alipoteza mchezo huo wa fainali dhidi ya Hakizumwami Junior wa Rwanda kwa seti 2-0 za 6-2 na 6-4.

Mchezo huo uliofanyika kwa saa 2:10 uliwavutia mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kutokana na upinzani wa pande zote mbili huku mashabiki wa Rwanda na Tanzania wakipokezana kushangilia kila mchezaji wa nchi yao alipochukua pointi.

Mtanzania alianza vizuri na kuonyesha utulivu wa hali ya juu dakika za mwanzoni huku Hakizumwami akionekana kumlalamikia mwamuzi ambaye alisimamisha mchezo na kumuonya.

Hata hivyo, Rashid alishindwa 'kuendeleza kasi aliyoanza nayo na kuruhusu kipigo cha seti 2-0.

"Medali ya fedha haikuwa kusudio langu, nilihitaji dhahabu ambayo hata hivyo haikuwa bahati yangu" alisema Rashid kwa masikitiko.

Akizungumzia mchezo huo, Hakizumwami alisema ulikuwa mgumu na alianza kuona dalili za kufungwa mwanzoni.

"Nilihisi kutoka mchezoni, lakini kocha na mashabiki walinituliza na kila waliponishangilia niliongeza juhudi zaidi," alisema.

Alisema licha ya ushindi amepata upinzani mkali kutoka kwa Rashid katika fainali hiyo ya vijana chini ya miaka 14.