MO Dewji abadili gia angani arudi Simba SC

Muktasari:

Mo aliandika ujumbe katika mitandao yake ya kijamii ambao ulisomeka kuwa ni aibu kwa klabu hiyo kushindwa kushinda huku akienda kwa mbali kwa kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kufuatia kulipa mishahara inayokaribia Bilioni 4 kwa mwaka.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji amerejea katika nafasi hiyo baada ya jana kutangaza kujiuzulu kutokana na klabu hiyo kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar.

MO amesema kilichotokea jana kwenye mitandao yake ya kijamii ilikuwa ni bahati mbaya hivyo bado yuko pamoja na timu hiyo na malengo yao yako pale pale ikiwemo kurudi kwenye ligi na nguvu zote.

Kupitia mitandao yake ya Kijamii, asubuhi ya leo, MO aliposti kwa mara nyingine tena, ujumbe usemao, "Kilichotokea kwenye akaunti zangu jana kilikuwa ni bahati mbaya, tuko pamoja, tunarudi kwenye ligi tukiwa na nguvu, tunajipanga kwa ajili ya ligi, nawapongeza Mtibwa kwa kuchukua kombe, mimi ni Simba damudamu, nitabaki kuwa Simba."

Hapo jana, Mo aliandika ujumbe katika mitandao yake ya kijamii ambao ulisomeka kuwa ni aibu kwa klabu hiyo kushindwa kushinda huku akienda kwa mbali kwa kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kufuatia kulipa mishahara inayokaribia Bilioni 4 kwa mwaka.

Mo aliamua kuchukua uamuzi wa kujiuzulu huku akiweka wazi kuwa ataendelea kusalia katika klabu hiyo kama mwekezaji na pia alisema ataendeleza miundombinu na soka la vijana.

Ujumbe wake wa kujiuzulu  ulizua hofu kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa Simba, akiwemo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye naye alitumia mitandao yake ya kijamii kuposti ujumbe uliosomeka, "Matokea ya Mpira huleta furaha na huzuni kwa wanaofungwa. Natoa pole kwa timu  yangu ya Simba pamoja na Mashabiki wote na wanaoitakia mema Simba. Sina uhakika na kinachoendelea kwenye Akaunti ya MO kama ni mwenyewe ameandika.

"Nawaomba wanasimba tutulie tutapata ukweli muda si mrefu. Tusisahau kuwa Wapo watu pia wabaya hutumia mwanya huu kuvuruga Amani na utulivu wa Team zetu. Simba nguvu moja."