Kete Taifa Stars kwa Guinea ya Ikweta iko hapa

Muktasari:

Winga Javier Balboa alikuwa miongoni mwa wafungaji bora wa fainali hizo ambazo Ivory Coast  ilitwaa ubingwa. Mara ya kwanza timu hiyo ilishiriki mwaka 2012 ilipoandaa kwa kushirikiana na Gabon.

Dar es Salaam. Licha ya Guinea ya Ikweta kucheza nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon),  ubora wa safu ya ushambuliaji  na ulinzi  ni mambo mawili yatakayoibeba Taifa Stars katika mchezo wa Ijumaa.
Taifa Stars itaikabili Guinea ya Ikweta katika mchezo wa Kundi J wa kufuzu fainali hizo utakaochezwa Uwanja wa  Taifa, Dar es Salaam saa 1:00 usiku.
Timu hizo zimecheza Afcon mara mbili kila moja. Guinea ya Ikweta inabebwa na historia ya kucheza nusu fainali ya mwaka 2015 ilipokuwa mwenyeji.
Winga Javier Balboa alikuwa miongoni mwa wafungaji bora wa fainali hizo ambazo Ivory Coast  ilitwaa ubingwa. Mara ya kwanza timu hiyo ilishiriki mwaka 2012 ilipoandaa kwa kushirikiana na Gabon.
Emilio Nsue wa Apollon Limassol ya Ugiriki ndiye mshambuliaji tegemeo wa Guinea ya Ikweta akiwa amefunga mabao 11 kati ya 17 ambayo imefunga katika mechi 10.
Licha ya mabeki wake kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 14, mawili yakiwa kwa penalti katika mechi 10, Nsue ndiye mkali wa mabao kati ya 11, matatu alifunga kwa penalti.

Rekodi
Guinea ya Ikweta katika mechi 10 za mwisho ilishinda tatu dhidi ya Sudan mabao 4-1, Chad 2-1 na Sudan Kusini 1-0, imefungwa  michezo miwili na  Saudi Arabia 3-2, RC Congo  1-0, ilitoka  sare tano dhidi ya Liberia 1-1, Chad 3-3, Sudan Kusini 1-1, Congo  2-2  na Togo  1-1.
Safu ya ushambuliaji ni hatari kipindi cha kwanza ambapo kati ya mabao 17 iliyofunga katika mechi hizo,  11 imefunga kipindi cha kwanza dakika ya 2, 3, 22, 32,19, 36, 11, 25, 34, 32 na 44. Mabao sita imefunga kipindi cha pili dakika ya 72, 63, 82, 71, 49 na 85.
Safu ya ulinzi imeruhusu mabao mengi kipindi cha pili ambapo kati ya 14 waliyofungwa, manane dakika ya 74, 90, 68, 83, 75, 54, 57, 52 na  sita kipindi cha kwanza dakika ya 29, 17, 20, 4,13,15.

Makipa
Ukiachana na Kelvin Yondani aliyecheza mechi 82 na Erasto Nyoni wa Sinba aliyecheza mechi 88, kipa Juma Kaseja anapewa nafasi kuibeba Taifa Stars kutokana na uzoefu wake langoni kulinganisha na Felipe Ovono anayecheza  Mekelle 70 Enderta ya Ethiopia.
Kaseja amecheza mechi 62 na  kipa wa Guinea ya Ikweta Ovono  38.

Kauli za wadau
Katika mchezo huo wadau wameipa Taifa Stars mchongo wa kufanya vizuri  ambapo kocha Kenny Mwaisabula alisema timu hiyo ina nafasi ya kushinda kama wachezaji wataamua.
Kocha wa Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard alisema Taifa Stars ikitulia na kucheza kwa umakini itapata ushindi.
“Morali ya Watanzania kwa timu ya Taifa ni kubwa hiyo ni hamasa tosha, pia wachezaji wetu wa kulipwa wamekuwa na mchango mkubwa wakishirikiana na wale wanaocheza nyumbani naamini kama watakuwa makini wana uwezo wa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema.
Mchambuzi Ally Mayay alisema  Guinea ya Ikweta si timu nyepesi, lakini kama Taifa Stars itaweka nia ya kushinda nafasi ipo na utakuwa mwanzo mzuri wa kufuzu Afcon.

Kocha, TFF wafunguka
Wakati rais wa TFF, Wallace Karia akisema mipango ni kufuzu mara ya tatu kucheza Afcon, safari hiyo itaanza Ijumaa, kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema anaamini watakuwa na mwanzo mzuri katika mechi hiyo.
Ndayiragije aliyeiongoza Taifa Stars kucheza fainali za Chan 2020 alisema ameiandaa timu kwa kiwango bora. “Tunachohitaji ni kuanza vizuri kwa kupata ushindi  nyumbani vijana wangu hawatoniangusha,” alisema Ndayiragije.
Karia alisema mkakati ni kuiandaa Taifa Stars kushiriki mashindano yote ya CAF kwa kiwango bora na baada ya kufuzu Chan wameelekeza nguvu katika mchezo dhidi ya Guinea ya Ikweta.