Kabwili: Yanga hatujaikimbia Simba SC, ila Mtibwa Sugar wazuri

Muktasari:

Mtibwa Sugar baada ya kuiondoa Yanga katika mechi ya nusu fainali wametinga fainali na wanasubiri mshindi wa nusu fainali ya Simba na Azam ambayo itachezwa leo Ijumaa saa 2:15 usiku itachezwa mechi ya fainali Januari 13, 2020 kwenye Uwanja wa Amaan.

Dar es Salaam.Kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili amesema kuondolewa na Mtibwa Sugar katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar si kama wamewakimbia wapinzani wao Simba bali ni matokeo ya mchezo tu.

Kabwili alisema si kama wamewakimbia Simba kama mashabiki wengi ambavyo wanadhani bali walijipanga kushinda katika mechi ya nusu fainali, lakini Mtibwa Sugar walionekana kujipanga vyema na kusawazisha bao na wakaenda kushinda penalti.

"Kwanza siyo kama tungeshinda ndio tungekutana na Simba kwani nao walikuwa wanacheza na timu kubwa ya Azam na yoyote angeshinda hapo ndio tungecheza naye kwa maana hatukuikimbia Simba bali tulipoteza kutokana na matokeo ya mpira yalivyo," alisema.

"Yanga ni timu kubwa ambayo inahitaji mataji mengi kwa maana hiyo kuondolewa katika kombe hili si jambo zuri kwetu kwani malengo yetu yalikuwa kuchukua ubingwa na tulijiandaa kushindana na timu yoyote hile," alisema Kabwili.