Jaji Mtulya ashinda mbio za kukimbia na ndimu

Muktasari:

Michezo iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho kuwa ni kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kushindana kula mkate mmoja wa boflo (slesi) na coca, mbio za mita 100, kukimbia na magunia, kukimbia na ndimu, pool table, mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa pete (netiboli)

Tanga.Tamasha la Michezo la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga limefana kwa kumshuhudia Jaji wa Mahakama  Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Fahamu Mtulya akishinda mbio za mita 80 za kukimbia na ndimu kwenye kijiko.

Jaji Mtulya yupo IJA kwa ajili ya mafunzo ya waheshimiwa majaji, ameteuliwa kuwa Jaji na Rais Dk. John Magufuli, Januari 27, mwaka huu, aliwashinda wenzake zaidi ya 20 wakiwemo watumishi wa Mahakama na wananchi na kujishindia sh20,000.

Jaji Mtulya aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto anayeshughulikia Utafiti, Taaluma na Ushauri, alisema amefurahi kwa kupata fursa ya kushiriki Bonanza hilo, na kupata zawadi hiyo.

Bonanza hilo liliwashirikisha watumishi wa Mahakama, wananchi, wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi, chekechea na sekondari ikiwemo wenye ulemavu wa akili kutoka Irente.

Mratibu wa Bonanza hilo ambaye pia ni Afisa Mahusiano na Habari wa Chuo cha IJA, Aristarch  Kiwango, alisema bonanza hilo linafanyika kila mwaka, na nia ni kuwakutanisha watumishi na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi, na kushiriki nao kwenye michezo mbalimbali, ikiwa ni kujenga mahusiano mema.

"Pamoja na kujenga mahusiano mema, pia ni kuweka fiti afya za watumishi wa Mahakama ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi. Pia ni katika kuwaweka wananchi karibu na Taasisi ya IJA ili kujiona wao ni sehemu ya chuo hiki" alisema Kiwango.

Kiwango alitaja baadhi ya michezo iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho kuwa ni kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kushindana kula mkate mmoja wa boflo (slesi) na coca, mbio za mita 100, kukimbia na magunia, kukimbia na ndimu, pool table, mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa pete (netiboli).