Muivory Coast wa Yanga apania kuitungua Kagera Sugar leo

Wednesday January 15 2020
Ivorypic

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Yikpe Gnamien amepanga kufungua akaunti yake ya mabao Ligi Kuu Bara katika mchezo wa leo dhidi ya Kagera Sugar.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Yanga kwa kusaini mkataba wa miaka miwili, alisema amezoeana na wachezaji wenzake hivyo ni matarajio yake kufanya vizuri katika mchezo huo, utakaochezwa Uwanja wa Uhuru.

"Sina shaka na nilionalo katika kufunga. Nipo tayari kutoa mchango wangu kwa ajili ya kuisaidia timu kufanya vizuri," alisema Yikpe ambaye alipewa jezi namba tisa.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast, anatarajiwa kukutana na upinzani wa kuwania namba ya kucheza kikosi cha kwanza na Ditram Nchimbi aliyetokea Polisi Tanzania, David Molinga, Tariq Seif ambaye kwa sasa ni majeruhi na Bernard Morrison aliyetambulishwa jana usiku.

Yanga wapo nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 25, walizokusanya katika michezo 12, Kagera Sugar ya Mecky Maxime ipo nafasi ya tisa wakiwa na pointi 24, wamecheza michezo, 16, utofauti wa pointi baina yao ni moja.

Kagera Sugar ambao waliisumbua Simba msimu uliopita  kwa upande wa Yanga walishindwa kufua dafu kwani  walipoteza katika michezo yote miwili, wa kwanza wakiwa nyumbani, Novemba 25, 2018 walichapwa mabao 2-1, wakiwa ugenini, Aprili 11, 2019 wakapoteza tena kwa mabao 3-2.

Advertisement

 

 

 

Advertisement