Glazer akata mzizi wa fitina Solskjaer haondoki Manchester United

Muktasari:

Hata mashabiki wa Man United wale waliokuwa wakipiga kelele za kumtaka Solskjaer afukuzwe, wameanza kumsapoti kocha wao na kuamini kumbe kuna kitu anaweza kukifanya.

Manchester, England. Manchester United imewambia Ole Gunnar Solskjaer kibarua chake kipo salama hawana mpango wa kumchukua Mauricio Pochettino.

Kauli hiyo ya Manchester United inatokana na kikao baina ya Joel Glazer na kocha Solskjaer huku akihakikishiwa kupewa fedha za usajili wa kiungo wa Atletico, Saul Niguez.

Manchester United imechukua uamuzi huo baada ya ushindi dhidi ya Tottenham na Manchester City na kuwapandisha hadi nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England na kufufua matumaini yao ya kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.

Uamuzi huo unamfanya Ole Gunnar Solskjaer amepindua meza, ndicho unachoweza kusema. Unajua kwanini, siku nne zilizopita, jina la kocha Mauricio Pochettino lilikuwa likitajwa karibu kila dakika na kuhusishwa moja kwa moja na kibarua cha kwenda kuinoa Manchester United.

Lakini sasa kocha huyo wa zamani wa Tottenham itabidi atafute kazi tu kwingineko, Old Trafford hakuna nafasi kabisa kwa siku za karibuni.

Katika mechi tatu baada ya Pochettino kufutwa kazi huko Spurs, Man United walikuwa kwenye hali mbaya, hawakuwa wameshinda yoyote, tena wakicheza na timu mbili zilizopanda daraja kwenye Ligi Kuu England pamoja na klabu ndogo ya huko Kazhakhstan, Astana.

Jambo hilo liliwafanya hata mashabiki waliokuwa kipenzi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kuanza kutia shaka kama kweli anastahili kuendelea kubaki kwenye timu yao. Hali ilifikia mbaya zaidi baada ya kutambua kwamba Pochettino hana kazi na anaweza kupatikana kirahisi ikiwa ni kocha waliyekuwa wakimtaka huko nyuma wakati walipomfuta kazi Jose Mourinho kabla ya kumleta Solskjaer.

Man United ni kama ilikuwa imetegesha kwenye mechi mbili zilizokuwa zikifuata kwamba matokeo yoyote ya kipigo basi ingekuwa habari mbaya kwa Solskjaer licha ya kwamba bosi kubwa, Ed Woodward amekuwa akimhakikishia usalama kocha huyo. Lakini, Solskjaer amepindua meza.

Aliingia kwenye mechi hizo mbili za Ligi Kuu England dhidi ya makocha mahiri Jose Mourinho na Pep Guardiola na zote ameshinda, akiishapa Spurs uwanjani Old Trafford na kisha kuikung'uta Man City kwao Etihad.

Jambo hilo linamwondoa kabisa Solskjaer kwenye presha ya kupoteza kazi na sasa Pochettino atafute tu ajira kwingineko kwa wakati huu Old Trafford hakuna nafasi hasa ukizingatia kwamba bosi Ed Woodward alisema hadharani akimuunga mkono kocha wake wakati alipochapwa na Newcastle United, Oktoba.

Hata mashabiki wa Man United wale waliokuwa wakipiga kelele za kumtaka Solskjaer afukuzwe, wameanza kumsapoti kocha wao na kuamini kumbe kuna kitu anaweza kukifanya. Solskjaer ndiye kocha pekee aliyepata pointi msimu huu kwenye mechi dhidi ya Liverpool huku akiwa amewapiga wababe wengine pia kama Chelsea, Leicester City, Spurs na Man City. Lakini, kitu cha kushangaza timu hiyo imepoteza pointi kwenye mechi dhidi ya Newcastle, Sheffield United na Aston Villa. Yote kwa yote, Man United wanaanza kuamini upya katika mapinduzi ya Solskjaer jambo linalowafanya kutokuwa na haraka ya kumfikiria Pochettino.