Dodoma Jiji FC wamlilia mjumbe wao, simanzi yatawala

Tuesday January 7 2020

Mwanaspoti-Dodoma-Tanzania-wamlilia mjumbe wao-Kifo-simanzi-yatawala

 

By Matereka Jalilu

Dodoma. Simanzi na vilio vimetawala nyumbani kwa aliyekuwa Afisa Utamaduni na michezo wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Mwalimu Chishosha William aliyefariki jana Jumatatu msiba upo nyumbani kwake Nkuhungu jijini hapa.

Marehemu Chishosha alifariki kwa ajali ya gari katika eneo la Mbande nje kidogo ya jiji la Dodoma wakati akirudi kutokea Dar es Salaam. Taarifa za awali zinaeleza marehemu atazikwa katika makaburi yaliyopo eneo la Ipagala jijini Dodoma.

Taarifa za kifo chake kimegusa makundi mbalimbali ikiwemo wasanii, wanamichezo na wapenda sanaa kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa aliokuwa anautoa kwao akiwa kiongozi wao anayewawakilisha.

Mbali na hayo, Marehemu Chishosha alikuwa ni Mjumbe wa kamati ya utendaji wa timu ya Dodoma Jiji FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

Afisa habari wa Dodoma FC, Ramadhani Juma alisema ni pigo kwao kumpoteza kiongozi huyo kutokana na ushiriki wake mkubwa na hamasa aliyokuwa nayo kwa ujumla.

"Tumehuzunishwa na msiba wa mwenzetu kuanzia jiji pamoja na timu kutokana na mchango wake mkubwa hususani hamasa yake na hata kusafiri na mashabiki kutimiza mchango wake," alisema Juma

Advertisement

Mashabiki wa timu hiyo ya jiji, Jackline Chaula kwa niaba ya wenzake alisema wamempoteza kiongozi na mdau mwenzao wa kusafiri pamoja kuihamasisha timu hiyo kupata matokeo ya kila mechi.

"Kiukweli tumepoteza mtu muhimu sana kwetu kama kikundi rasmi cha timu kwa sababu alikuwa pamoja nasi kwenye kuhamasisha timu kushinda katika mechi za timu yetu na alitupatia ngoma za kuhanikiza uwanjani," alisisitiza Chaula.

Advertisement