Aussems: Huyu Sheva ni Samatta mwingine, Ajibu hapana

Monday December 9 2019

Mwanaspoti-Aussems-Tanzania-Huyu-Sheva-Samatta-mwingine-Ajibu hapana

 

By KHATIMU NAHEKA

Dar es Salaam. Aliyekuwa Kocha wa Simba, Patrick Aussems na alifunguka mengi ikiwamo anavyowajali wachezaji na alivyotimua baadhi ya viongozi wa klabu hiyo waliokuja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mechi na Yanga.
Leo katika sehemu hii ya mwisho, kocha huyu ambaye kwa sasa yuko nchini kwao Ufaransa baada ya kusitishiwa mkataba anaendelea kujibu maswali na kuelezea mambo mbalimbali yalivyokuwa wakati akiwa ndani ya wekundu hao.

Aliambiwa nini aliposimamishwa
“Nakumbuka ilikuwa ni Jumamosi, waliniita na kunikabidhi barua ya kusimamishwa ikiwa na mambo yote waliyoyaeleza, lakini katika maelezo yao kulikuwa na sababu kama mbili ambazo sikukubaliana nao, mengine yalikuwa sawa, kwa hiyo kuanzia hapo nilielewa mpango wao sasa unakaribia kukamilika.
Wachezaji walimwachia ujumbe gani baada ya kufukuzwa
“Niwe muwazi wachezaji waliumizwa na hatua hii na wengi wamekuwa wakiniamba nisiwasahau katika hatua yoyote yangu inayofuata baada ya kutoka Simba kama nitapata timu mpya haraka. Wameniambia bado wanatamani kufanya kazi na mimi, kwangu mimi ni kawaida hasa unapokuwa katika kundi la watu kama nilioishi nao ambao wengi wao wana kiu ya kupata mafanikio zaidi.
“Unajua hapa Simba kuna watu wachache ambao wana ndoto kubwa za kuendelea kufanya kazi lakini kwa wachezaji wengi wazawa shida yao kubwa wanapenda zaidi kuwa mastaa hapahapa kwao na sio kwenda kutafuta changamoto kubwa nje ya nchi.
“Nina marafiki wengi Ufaransa na Ubelgiji lakini wale wa ubelgiji wengi wao baada ya kuona mafanikio ya Samatta (Mbwana) wanatamani kuona wanamtoa Samatta mwingine mmoja au zaidi hapa na majibu yangu yanakuwa wapo ambao wanaonyesha ubora kama huo kama wakija.”

Mchezaji gani anaona anaweza kuwa Samatta mpya
“Nafikiri Miraji (Athuman ‘Sheva’) anaweza kuwa na ubora huo kwa mambo ambayo anayafanya sasa ukilinganisha na umri wake. Kama ataendelea kujitunza na kuwa na malengo ya mbali, pia itategemea na makocha watakaokuja kama watamwendeleza zaidi.”

Vipi kuhusu Ajib?
Akizungumzia ubora wa mshambuliaji Ibrahim Ajibu kama anaweza kuwa staa mkubwa Ulaya na wapi anakwama Aussems alisema:” Kwa mpira wa Ulaya niseme wazi Ajib hapana, hataweza kwa jinsi alivyo sasa na nilivyomwona tangu alipokuwa nje na hata ndani ya Simba, sababu kubwa inayomharibia ni mvivu sana, hulka yake na hata mwili wake.
“Anapokuwa na mpira Ajib ni habari nyingine anakuwa ni hatari sana na hakuna anayeweza kumgusa akiwa nao kwa ubora, lakini shida inakuja anapokuwa hana mpira, anawaachia wenzake jukumu zima la kumkabia, kwa mpira wa sasa hilo hakuna timu itakayokubaliana na mchezaji wa namna hiyo.

Alijaribu kumbadilisha?
“Nimeongea naye sana alipofika Simba anatakiwa kucheza kwa nidhamu ile ile ya kama anapokuwa na mpira, pia akipoteza anatakiwa kuwa na jukumu la kufanya katika kuutafuta, naona ni hatua ngumu kidogo kumbadilisha.

Ujumbe gani aliwaachia wachezaji wake
“Mimi niliwaambia najua wazi najua wengi wenu waliumizwa na hatua ya kufutwa kwangu kazi na hawakuelewa kwa sababu tulikuwa tunaongoza ligi, tunacheza mpira wa kuvutia ingawa tulikuwa tuna majeruhi wengi, lakini nikawaambia kuondoka kwangu kusiwakatishe tamaa waendelee kujituma, pia watambue mchezo ujao baada ya mwezi mmoja nafikiri itakuwa mwakani watakutana na Yanga, hii ni mechi kubwa na itakuwa na ya aina yake, nimewaambia kama kuna kitu watanifurahisha basi nije nisikie wamechukua ubingwa.
“Hawatakiwi kuhuzunika sana kwa kuwa hata mimi naondoka nikiwa natabasamu ni kutokana na wao nawaacha wakiwa salama na ubora mzuri katika ushindani wanatakiwa kuendelea na maisha.”

Anajua anaitwa Uchebe
Moja ya jina kubwa ambalo wadau wa Simba na hata nje ya Simba walikuwa wakimwita jina la Uchebe hapa anaelezea hilo na alivyolipokea: “Ndiyo najua wananiita uchebe, (anacheka kidogo),najua hilo kila ninapopita utaona wananiita uchebe na hata katika mitandao wananitambulisha hivyo na sio kocha wala Patrick nafikiri labda nikiondoka nitakata hizi ndevu zangu ambazo nasikia ndio asili ya hilo jina.
“Niliposikia kwa mara ya kwanza wananita hivyo nikajaribu kutafuta kwa nini wananiita hivyo, ina maana gani, nilipojibiwa ni kutokana na ndevu zangu na haikuwa na maana mbaya nikasema hakuna shida acha waendelee kuniita hivyo ni sehemu ya maisha.”

Amejifunza nini Tanzania
“Tanzania ni nchi nzuri sana kitu ambacho nitakikumbuka ni jinsi watu wa hapa wanavyoishi kwa upendo. Ni ngumu wakati mwingine kupata sehemu nzuri yenye amani kama ilivyo hapa, hiki nasema kwa Watanzania wote nawashukuru sana kwa hili nimejifunza mengi, sio tu kufanya kazi hapa bali hata kuishi hapa, usishangae kuniona hapa. Wakati mwingine naweza kuja kuishi tena hapa hili nakuhakikishia.”

Tukio gani liliwahi kumuumiza
“Tangu nimekuwa hapa mara nyingi sijawahi kukutana na wakati mgumu lakini tukio ambalo liliniumiza ni wakati ule MO amepata matatizo.
“Ulikuwa wakati mgumu sana kwangu kwa kuwa MO ni mtu mwenye pesa, pia ni muungwana sana, kwa sasa namwona anarudi katika hali yake taratibu lakini bado sio yule MO ambaye alikuwa hapo kabla nafikiri lile tukio lilimumiza sana haikuwa ngumu peke yake hata mimi liliniumiza sana.”

Advertisement