Ukweli ndivyo Ulivyo! Yanga isipaniki, ichague moja tu!

Sunday February 23 2020

Mwanaspoti, Yanga, Eymael, Simba, Tanzania, Mwanasport, Michezo, Ligi Kuu, mechi,

 

By Badru Kimwaga

SIO siri, kwa sasa mashabiki wa Yanga hawana furaha. Wamepoteza ile bashasha waliokuwa nayo awali. Wamekosa amani mioyoni mwao, hata kama wanajikaza kisabuni.
Ndio, watakuwaje na furaha wakati chama lao linayumba? Yanga haifanyi vyema uwanjani kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara.
Watakuwaje na raha wakati kasi ya watani wao wa jadi, Simba katika kunyatia ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo ipo juu?!
Kasi hiyo ya watani wao imewanyo ng’onyesha kabisa. Mbaya zaidi hata wale nyota wao waliowapa jeuri kipindi cha usajili wa dirisha dogo na kutua Jangwani, wamewaangusha.
Walitarajiwa wangeleta mabadiliko kikosini, lakini wengi wao ni kama  wameyumba na kuwanyima raha! Ni ngumu kuwa na furaha, hata kama Bernard Morrison anawafariji kwa lile soka lake tamu na la nguvu lililowakata stimu kwa muda mashabiki wa Simba. Unabisha nini?
Simba walinywea baada ya Morrison kuonyesha shibobo zake uwanjani. Ndio, maana kwa sasa unasikia upande wa pili nao wakimnadi Luis Jose Miquissone kama njia ya kuwanyamizisha watani wao.
Ndivyo soka la Kibongo lilivyo. Mashabiki wanafurahia udambwi dambwi hata kama hauna tija ndani ya timu. Wao furaha yao ni kunyamazishana mitaani. Kwa sasa wadau wa soka wanasubiri tu kuona pambano lao la Machi 8, litakuwaje, nani atamzima mwenzake?
Lakini mpaka sasa ukweli ulivyo mashabiki wa Yanga wameshakata tamaa ya ubingwa.
Wameshamkatia tamaa Yikpe Gnamein ambaye waliamini angekuwa kama Emmanuel Adebayor. Sawa kafunga mabao mawili, lakini amepoteza nafasi nyingi za wazi ambazo kama angekuwa na shabaha na kuzitia nyavuni, ingeisaidia Yanga kuokoa pointi ilizodondosha katika sare ilizopata.
Sare tatu mfululizo ilizopata Yanga kwenye mechi zao zilizopita, imewaweka katika nafasi ngumu ya kuwasogelea watani wao Simba.
Kabla ya mchezo wa usiku wa  jana, Simba ilikuwa imeiacha Yanga kwa alama 19. Ni pointi nyingi mno. Sawa, Yanga ina michezo miwili mkononi, lakini bado haiwapi uhakika wa kuzikusanya alama zote sita katika mechi hizo za viporo. Mwenendo wao unawaangusha.
Inawezekana Yanga kwa sasa ikajilaumu chini kwa chini, uamuzi wao wa kumleta Kocha Luc Eymael.
Ndio, chini ya Kocha Mwinyi Zahera ndani ya msimu huu, Yanga ilitepeta. Wakamtoa na kumpa kwa muda Charles Boniface Mkwasa. Nyota huyo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania.  Aliiongoza vyema Yanga na kuvuna pointi za kutosha zilizowapa matumaini ya kuwajongelea watani wao.
Sare ya mabao 2-2 ilichochea zaidi mzuka kwa mashabiki na hata mabosi wao, wakiamini mnyama alikuwa bado kidogo kunaswa Jangwani.
Lakini mambo yamebadilika chini ya Eymael. Tayari wameshapoteza mechi mbili na kuvuna sare tatu mfululizo. Haijulikani leo kule Mkwakwani, jijini Tanga litatokea nini, lakini soka ndivyo lilivyo.
Huwezi kumlaumu Eymael. Soka sio kama chumvi ambayo ukiikoroga kidogo tu kwenye mboga inakolea. Soka ni mchezo unaohitaji muda wa mwalimu kulisha falsafa zake kwa wachezaji.
Mbaya ni nyota waliokuwa wameanza kuzoeana chini ya Zahera na hata Mkwasa, wameyumbishwa kwa vile baadhi ya wenzao walitimka kikosini na kuletewa wapya. Bado hawajazoeana, lakini wale waliokuwa vinara enzi za makocha waliotangulia kwa sasa wanachomeshwa mahindi katika benchi.
Kwa namna hiyo, ni dhahiri Yanga hawana sababu ya kupaniki ama kuanza kumsaka mchawi. Wakubali tu hali halisi hata msimu huu hawana chao katika Ligi Kuu, lakini bado kama chama lao lina nafasi ya kufanya kupitia Kombe la FA.
Keshokutwa wataikaribisha Gwambina FC katika mechi ya 16 Bora. Huu ndio mchezo muhimu kwao kama kweli wanataka kuipata tiketi ya michuano ya kimataifa msimu ujao. Kama watafanya kosa mbele ya wababe hao wa FDL, wajue itakula kwao.
Ukweli ndivyo ulivyo, nafasi pekee ya Yanga kuiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika ipo FA, tena sio kirahisi ni lazima ipambane ikianzia kwa Gwambina na wapinzani wengine watakaopangwa nao katika hatua zinazofuata za Robo Fainali hadi Fainali kama watafanikiwa kuvuka.
Hata kama ni kweli soka ni mchezo wa maajabu, lakini hesabu zinawakataa mapema kwenye Ligi Kuu, japo hawapaswi kukata tamaa.
Hii ni kwa sababu ya ubora wa wapinzani wao wanaotetea taji, pia kwa mwenendo wao wa kusuasua na kwa vile mshika mawili moja mponyoka, Jangwani waangalie mlango rahisi wa kuwapeleka CAF vinginevyo, watatoka kapa tena kama msimu uliopita!

Advertisement