EXTRASPESHO: Konde Boy anazitaka himaya za Diamondi, Kiba

Sunday March 22 2020

Mwanaspoti, Team Diamond, ni Team Kiba, Harmonize kupata somo

 

By Amour Hassan

KWA miaka mingi sasa gemu ya Bongofleva imekuwa ikitawaliwa na Diamond Platnumz na Ali Kiba.
Ushindani wa masupastaa hawa wawili wa muziki wa kizazi kipya nchini umekuwa ni kama ule wa timu za soka za Simba na Yanga -- yaani wewe kama si Team Diamond, basi ni utajikuta tu ni Team Kiba.
Iko hivyo yaani, mitaani kote. Watu wanakuwa wanampenda tu staa wao na kumtetea kwa kila jambo. Akitoa ngoma mbovu, kamwe hiyo haitoshi kuwafanya wahamie timu ya mpinzani wao.
Sasa ngoja akosee jambo la kimaisha mpinzani wao... atakoma! Watamnyooshea vidole hadi aione dunia chungu. Lakini kesho yake tu afanye kosa kama hilo staa wao, utawasikia, “Naye pia ni binadamu. Asikosee kwani yeye malaika?” Ndivyo walivyo mashabiki wa timu hizi.  Hali hii imekuwa hivi kwa miaka mingi na imeonekana ni ngumu mtu kuingia kati yao na kutingisha himaya hizi imara. Lakini tangu kujitoa kwa Harmonize katika lebo ya WCB na kuanzisha lebo yake ya Konde Gang, manyunyu tayari yameanza kuonyesha dalili za mvua.
Konde Boy ni tishio kwa himaya hizi. Huo ndio ukweli. Kulelewa katika lebo ya Diamond kumemjenga sana Konde Boy. Kufanya kazi miaka kadhaa na Wasafi kumemfanya Harmonize kupata somo la ni vipi biashara ya muziki inafanyika. Hii ni kuanzia kujibrand yeye mwenyewe kama msanii mkubwa hadi kufanya kazi za hadhi ya msanii mkubwa.
Haya ni mafunzo na silaha muhimu aliyotoka nayo Konde Boy kutoka katika kambi ya ‘jeshi lenye mafanikio’ la WCB.
Na onyesho lake alilofanya wiki iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City ni ishara kwamba Konde Boy anatishia himaya hizi mbili kubwa za Team Kiba na Team Mondi.
Uchapakazi wa Konde Boy, ambaye ametoka mbali kufika alipo (ikiwamo kuanzia kuuza kahawa mitaani Kariakoo hadi kukataliwa katika mashindano ya Bongo Star Search), unaweza kumfikisha mbali.
Ni kweli kwamba aliibuliwa na Diamond. Ni kweli kwamba alikuwa akimuiga Mondi kwa kila kitu kuanzia kuimba, kuongea, kucheka, kucheza hadi mapozi ya picha hadi watu kumkosoa sana mitandaoni na kwenye vyombo vingine vya habari.
Lakini watu wanapaswa kutambua kwamba ukimuiga Cristiano Ronaldo anavyoishi, nidhamu yake ya mazoezi na anavyocheza mpira na ukafanikiwa kupata japo robo tu ya uwezo wake uwanjani, wewe tayari ushatoboa kimaisha katika soka. Iko hivyo kwa Konde Boy ambaye tayari sasa ametoboa. Kumuiga Mondi ilikuwa ni katika kusaka njia ya kutokea na sasa ameshapata staili zake tofauti (hata kama sio sana) na anachanja mbunga.
Lakini kuzitingisha himaya za Mondi na Kiba si jambo jepesi hata kidogo. Hawa jamaa wawili pamoja na vipaji na nidhamu walivyonavyo katika muziki, wameweza kudumu katika chati za juu kwa zaidi ya miaka 10 wakiachia ngoma kali baada ya nyingine.
Hapa ndipo ulipo mtihani mkubwa zaidi. Lionel Messi na Ronaldo wamekuwa wakizungumzwa wao tu kila siku katika soka si kwa sababu hamna wakali wengine wanaoibuka na kutishia himaya zao, bali ni kwa sababu wamedumu katika ubora wao kwa zaidi ya miaka 10.
Tatizo linalowafanya wasanii wengi kushindwa kutingisha himaya za Mondi na Kiba ni kushindwa kutoa ngoma kali mfululizo kwa miaka mingi. Wengi wao licha ya kuibuka na upepo mkali, hukata pumzi mapema na kushindwa kutamba katika ‘ruti ndefu’ ya marathon za Mondi na Kiba. Lakini Konde Boy analeta kila matumaini kwamba anaweza kuingia pale katikati ya masupastaa hawa wawili. Onyesho lake la hadhi ya juu la uzinduzi wa albam yake ya ‘Afro East’ kwenye Ukumbi wa Mlimani City wiki iliyopita limeonyesha kila dalili kwamba jamaa ni ‘next big thing in town.’ Fikiria kufanya onyesho kama lile pale Mlimani City na watu waingie kwa kadi za mwaliko tu! Na hata lile onyesho alilofanya kwao Tandahimba kwa kiingilio cha Sh.10,000 na mashabiki kufurika uwanjani katika mkesha wa Mwaka Mpya, ni ishara jamaa yuko ‘level’ zilezile.
Advertisement