Mashabiki wa Manchester United mpo! Solskjaer anatengeneza jeshi la kufa mtu

Muktasari:

Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka kutengeneza kikosi chake kuundwa na wachezaji vijana ili watumike kwa muda mrefu.

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER United tayari imeshaanza kuufanyia kazi mpango wake wa kufanya usajili mkubwa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu kwa kuwaweka Jack Grealish, James Maddison na Jadon Sancho kwenye orodha ya mastaa inaotaka kuwasajili.
Makamu mwenyekiti mtendaji wa klabu hiyo, Ed Woodward ametangaza wazi Man United itamwaga pesa kutengeneza kikosi chake kuwa kwenye ubora mkubwa.
Tayari timu hiyo imeshafanya usajili wa mastaa watano kutengeneza kikosi hicho akiwamo Daniel James, Aaron Wan-Bissaka, Harry Maguire, Bruno Fernandes na Odion Ighalo, ambaye atapita tu na mkopo wake utakapokwisha ataondoka.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka kutengeneza kikosi chake kuundwa na wachezaji vijana ili watumike kwa muda mrefu.
Kama mastaa hao watatu, Grealish, Maddison na Jadon Sancho basi kikosi cha Man United kwa msimu ujao kitakuwa balaa kubwa.
Golini kama kawaida atakuwa David de Gea, ambaye atalindwa na ukuta wa mabeki Aaron Wan-Bissaka upande wa kulia, Victor Lindelof na Harry Maguire watacheza beki ya kati na kushoto atacheza Brandon Williams.
Kikosi hicho kitakachotumia fomesheni ya 4-3-3, katikati, kiungo mkabaji atakuwa Scott McTominay, akisaidiana na viungo wengine wa kati, Bruno Fernandes na Jack Grealish huku Paul Pogba akiondolewa kabisa kwenye kikosi.
Kwenye fowadi, winga ya kulia atakuwa Sancho kushoto ni Marcus Rashford na straika ni Moussa Dembele. Mastaa wengine kama Anthony Martial, Fred na wakali wengine wanaotamba kwa sasa kwenye kikosi cha kwanza wataanzia kwenye benchi.