Makocha wa Teqball wajifua kwa vitendo

Sunday February 16 2020

Mwanaspoti, Makocha wa Teqball, Tanzania, Mwanasport, Michezo, Michezo Blog

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Makocha 18 wa mchezo mpya nchini wa Teqball wamepewa semina ya sheria na kanuni za mchezo huo huku wakichuana wenyewe kwa wenyewe.

Semina hiyo ya siku mbili imefungwa leo Jumapili kwenye viwanja vya Filbert Bayi, Kibaha Mkuza mkoani Pwani ikiongozwa na makamu wa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Makocha kutoka mikoa ya Pwani, Mtwara, Iringa, Tanga, Shinyanga, Dar es Salaam, Tabora na Dodoma walijifunza mambo mbalimbali ikiwamo sheria za Teqball ambao ni mchezo wa soka ya mezani inayochezwa kwa kutumia kichwa na miguu pekee.

Mkufunzi wa mchezo huo ambao huko kwenye programu ya FutballNet inayosimamiwa na Taasisi ya Olympafrica na kufadhiliwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) na klabu ya Barcelona ya Spain, Damian Chonya alisema unachezwa kwa seti tatu.

Alisema timu moja inakuwa na wachezaji wawili na wakati mwingine anaweza kuwa msichana na mvulana na marefarii wanakuwa watatu.

"Kila seti ina pointi 20 na atakayezifikisha wa kwanza ndiye mshindi wa seti," alisema.

Advertisement

Makamu wa rais wa TOC, Henry Tandau alisema kwa Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi ya kwanza kucheza Teqball.

"Tumeanza mchakato wa kuufanya uwe mchezo wa kitaifa," alisema Tandau.

 

Advertisement