Mwanariadha Kipchonge awaza kuishangaza dunia kwa mara nyingine

Wednesday May 8 2019

 

By Thomas Matiko

MFALME wa Marathon, Eliud Kipchoge katangaza  kwa mara ya pili tena, atajaribu kukimbia mbio hizo chini ya muda wa saa 2:00.

Kwa maana hiyo, lengo lake ni kukata utepe kwa kusajili muda wa saa 1:59 au hata chini zaidi.

Hakuna mwanariadha yeyote duniani au katika historia ya mbio hizo zilizoanzishwa miaka 490 B.C (kabla ya Yesu Kirsto kuzaliwa), amewahi kutimka chini ya muda wa saa 2:00

Kipchoge mwenyewe anaishikilia rekodi ya dunia kwa muda wa saa 2:01.39, rekodi mpya aliyoiweka mwaka jana kwenye Berlin Marathon.

Jaribio hili la kutimka chini ya muda wa saa 2:00 litakuwa lake la pili baada ya kujaribu kwa mara ya kwanza 2017  jijini Monza, Italia alikoishia kukata utepe kwa  kusajili muda wa saa 2:00.25.

Licha ya kuwa rekodi ya kipekee, muda huo hautambuliwi na Shirikisho la Riadha duniani (IAAF) kutokana na vigezo vyake. Mwanzo Kipchoge aliruhusiwa kuwatumia wachochea kasi tangu mwanzo wa mbio hadi  mwisho, kitu ambacho hakipo kwenye Marathon ya kawaida. Pia aliwekwa kwenye lishe maalumu pamoja na kutungeneza njia nyepesi kwa ajili ya mbio hizo. Wakati huo jaribio hilo lilifadhiliwa na Breaking 2 na kuwahusisha wanariadha watatu pekee. Safari hii, jaribio hilo litafadhiliwa na bilionea mmoja wa Uingereza Jim Ratcliffe.

Advertisement

Akizungumzia mradi huo, Kipchoge ambaye atalamibishwa mkwanja mnene kwa kuhusika, alisema ndio kitakachokuwa kitu kikubwa zaidi yeye kuwahi kufanikisha katika taaluma yake ya riadha endapo atafanikiwa kusajili muda wa chini ya saa mbili.

“Kama nikifanikiwa kuweka rekodi hii, basi nafikiri ndicho kitakachokuwa kitu kikubwa zaidi katika taaluma yangu kwa sababu historia daima itanikumbuka, kuanzia kizazi cha sasa na vijavyo,” Kipchoge kafunguka.

Lengo la mbio hizi, sio kuweka rekodi mpya, bali kuonyesha uwezo wa mwili wa mwanadamu kutimka chini ya muda wa saa 2.

Advertisement