Mwanariadha Kipchoge aing’arisha Kenya kimataifa

Muktasari:

  • Kipchoge alituzwa kufuatia ufanisi wake wa kuweka rekodi mpya ya dunia kwenye mbio za Marathon kule Berlin, Ujerumani mwaka jana.

HIVI majuzi, staa mwanariadha mzalendo, Eliud Kipchoge alipokea tuzo ya heshima la Laures Exceptional Achievement Award kwenye hafla ya utoaji tuzo za michezo Laureus Sports Awards kule Monaco, Ufaransa.

Kipchoge alituzwa kufuatia ufanisi wake wa kuweka rekodi mpya ya dunia kwenye mbio za Marathon kule Berlin, Ujerumani mwaka jana.

Kwa kutunukiwa tuzo hiyo, Kipchoge anakuwa mtu wa nne kuipokea tangu zilipozinduliwa mwaka 2000. Awali Kipchoge alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo la mwanamichezo bora wa kiume wa mwaka, kwenye kitengo kilichowajumuisha mastaa wengine fowadi wa PSG, Kylian Mbappe, mwanavikapui LeBron James, kiungo wa Real Madrid Luka Modric na nyota wa tenisio Novak Djokovic aliyeibuka bingwa.

“Utambuzi huu una maana kubwa sana kwangu. Hii ina maana kuna kitu kikubwa ambacho nimekuwa nikikifanya duniani kiasi cha kutambuliwa sio tu kwenye kitengo cha riadha bali ni katika tasnia nzima ya michezo,” Eliud Kipchoge alifunguka baada ya kupokea tuzo hilo.

Mwaka jana Kipchoge 34, aliweka historia kwa kuwa mwanaridha ‘mkongwe’ zaidi kuwahi kuvunja rekodi ya dunia aliposajili muda wa saa 2:01.39 kwenye Berlin Marathon na kuipunguza rekodi ya awali yake Dennis Kimetto kwa sekunde 78.

Miezi minne kabla ya kuvunja rekodi hiyo, aliibuka mshindi wa London Marathon akisajili muda wa saa 2:04.17

Tayari ameanza kujiandaa kutetea ubingwa huo wa London Marathon mwaka huu na lengo lake ni kuibuka mshindi tena.

“Maandalizi yanakwenda vizuri sana. Ninachotaka ni kushinda London Marathon kwa mara ya nne” akaongeza.