Mwamuzi aambulia kichapo

Friday March 22 2019

 

By JUMA MTANDA,

 MOROGORO. WACHEZAJI wa Makipa FC Manispaa ya Morogoro wamemshushia kipigo mwamuzi wa kati Salum Mgaya baada ya kumtuhumu kuwapendelea wapinzani wao.

Mwamuzi huyo alikuwa akichezesha mchezo kati ya Home Boys FC na Makipa FC wa kusaka nafasi ya kutinga robo fainali mashindano ya Kombe la Pasaka 2019 yanayoendelea Uwanja wa Sabasaba mjini hapa.

Wachezaji hao walionekana kupuuza kanuni na sheria 17 za soka dakika ya 88 baada ya mwamuzi huyo kutoa adhabu ya penalti kwa wapinzani wao iliyozaa bao la kusawazisha.

Penalti hiyo ilitokana baada ya beki wa Makipa FC, Sadi Basi akiwania mpira na mshambuliaji wa Home Boys FC, Mboni Steven eneo la 18 ambapo hekaheka hizo zilitumika mchezaji wa Home Boys FC, John Joseph kunyanyua mikono juu kumjulisha mwamuzi kuwa beki huyo amefanya madhambi ya kushika mpira.

Mwamuzi alipuliza filimbi na kutoa adhabu hiyo kitendo kilichopingwa na wachezaji wa Makipa FC na kuanza kumfuata na kushambulia kwa kumpiga ngumu, makofi na mchezo huo kusimama kwa dakika mbili.

Baada ya sare hiyo ya bao moja mshindi alisakwa kwa mikwaju ya penalti kupata timu itakayotinga robo fainali ambapo Home Boys FC ilisonga mbeli kwa mikwaju 7-6 huku Makipa FC ikiaga mashindano hayo.

Advertisement

Mchezo huo ulikuwa wa kiporo baada ya mchezo wa awali kushindwa kumpata mshindi kufuatia dakika 90 kwenda sare ya bao 2-2 na katika penati siku hiyo zilipigwa 10 kila timu ikipata 9 na giza kuingia.

Katika mchezo huo, Makipa FC ilifunga bao lake dakika ya 20 lililofungwa na Salehe Libenanga lililodumu kwa dakika zote za kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

Mbali na matokeo hayo mchezo huo uliibua kituko kingine kabla ya kuanza ambapo mashabiki walimataka mwamuzi huyo abadilishe jezi ya juu kwani ilikuwa inafanana na jezi za wachezaji wa Makipa FC.

Timu zilizofuzu robo fainali hiyo ni Moro City FC, Palm SC, Moro Kids SC, New Kinds FC, Mawingu United, Home Boys FC, JL Academy SC na Tanzanite Academy.

Advertisement