Mwalala? Bandari kuna ngori

Muktasari:

Mkurugenzi huyo aliliambia Mwanaspoti timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri tangu msimu uliopita na kutokana na matokeo ya sawa kuwa mabaya, lazima kuna tatizo ambalo linastahili kutatuliwa kwa haraka.

MOMBASA, KENYA.KUMWACHISHA kazi Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala ama kuondoka kwake timuni hakutakuwa suluhisho la kuifanya timu hiyo ifanye vizuri kwenye mechi zake za Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Matamshi hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally aliyekuwa akijibu baadhi ya mashabiki waliotaka maofisa wa klabu hiyo wamuachishe kazi Mwalala kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo kwenye ligi ya msimu huu.

“Siwezi kuamini kuondoshwa kwa Mwalala (pichani kulia) kunaweza kuwa suluhisho la matokeo ya timu hiyo kuwa mazuri ila ningependekeza wazo la mkufunzi huyo la kukutana na wachezaji na maofisa wa klabu litiliwe maanani na lifanyike haraka,” akasema Baghazally.

Mkurugenzi huyo aliliambia Mwanaspoti timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri tangu msimu uliopita na kutokana na matokeo ya sawa kuwa mabaya, lazima kuna tatizo ambalo linastahili kutatuliwa kwa haraka.

“Mkutano ukifanyika na tatizo likijulikana na likatatuliwa, timu itarudia katika hali yake. Nawaomba mashabiki tuwe na subira kwani, nina imani tatizo lililoko litaweza kufanyiwa kazi na mambo yatakuwa shwari,” akasema Baghazally.

Mwalala mwenyewe alikiri baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na AFC leopards na kufungwa 2-0 na Gor kuwa kuna tatizo na amesema atakutana na wachezaji na viongozi wa klabu kulitatua tatizo ambalo hata hivyo, hakulitaja ni lipi.

Bandari ilishiriki kwenye dimba la Caf Confederation Cup na ikabanduliwa nje na timu ya Horoya AC ya Guinea kwenye mechi ya raundi ya nne ya kufuzu kwa mechi za marudiano.