Mwakyembe aota Kombe la Dunia

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema serikali inataka kuona Serengeti Boys inaandika historia kubwa kwa kufuzu Kombe la Dunia.


SERIKALI imeapa kufanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ inafuzu Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri huo zitakazofanyika nchini Peru baadaye mwaka huu.

Serengeti Boys ni miongoni mwa timu nane zitakazoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini mwezi Aprili ambapo timu nne zitakazofika nusu fainali zitafuzu Kombe la Dunia zitakazofanyika Oktoba.

Ushindi kwenye mechi mbili za kundi D la mashindano hayo, utaiwezesha Serengeti Boys kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufanya hivyo mwaka 2017 kwenye fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zilizofanyika Gabon.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema serikali inataka kuona Serengeti Boys inaandika historia kubwa kwa kufuzu Kombe la Dunia.

“Vijana wetu ni mabingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kusini, hivyo tunaamini wanakwenda kufanya mambo makubwa katika fainali za Afrika zinazofanyika hapa nchini.

“Watanzania waipe sapoti kubwa timu yao ili tuweze kubakisha kombe nyumbani na kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika Peru. Kwa upande wetu serikali tumejipanga vilivyo kuhakikisha vijana wanafanya vizuri na tuko tayari hata kuuza magari yetu ili tupate fedha za kuiandaa timu,” alisema Waziri Mwakyembe.

Serengeti Boys imepangwa kundi A pamoja na Nigeria, Uganda na Angola.