JICHO LA MWEWE: Mwakalebela katika wiki nyingine ngumu ya majaribu

Monday July 27 2020

 

By EDO KUMWEMBE

YANGA wameendelea kutupatia sinema za kufurahisha. Wiki iliyopita ilikuwa ni ya Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela. Sauti yake ilisambaa katika mitandao mbalimbali akidai kwamba, kama Yanga wamemchoka bora waachane kwa usalama.

Mwakalebela alimwaga mapovu kweli kweli. Nadhani alishtumiwa kwamba aliwahi kwenda Iringa kwa ajili ya kuihujumu Yanga katika pambano lao dhidi ya Lipuli. Mwenyewe anadai aliwahi mapema kumuuguza Mama yake mzazi.

Baada ya hapo sauti ya Mwakalebela ikaenda katika redio mbalimbali ikiwemo Wasafi. Ikazuka mijadala ya hapa na pale. Yote haya ni mwendelezo wa sinema zinazoendelea kila siku pale Yanga. Leo Bernard Morisson, kesho Papy Tshishimbi, keshokutwa David Molinga.

Ambacho ninamuonea huruma Mwakalebela ni kitu kidogo tu. Aliwahi kuongoza TFF kama Katibu Mkuu. Wakati ule bosi wake alikuwa Rais wa TFF, Leodeger Chilla Tenga. Huyu Mzee Tenga alitengeneza taasisi imara inayojielewa. Ilikuwa ni baada ya mnyukano wa muda mrefu uliotokana na uozo wa mabosi waliopita kabla yake.

Mwakalebela alikuwa na wakati mzuri TFF. Lakini pia kuna tofauti kubwa kati ya TFF na hizi klabu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga. Kuna kasheshe kubwa kuziongoza klabu hizi ambazo wanachama na mashabiki wana sauti kubwa.

Pale TFF hauongozi Simba na Yanga. Katika soka la uwanjani unaiongoza Taifa Stars. Kisha unasimamia Ligi. Kuiongoza Taifa Stars ni kazi nyepesi kuliko Simba na Yanga. Taifa Stars inaweza kufanya vibaya kwa miaka kumi na mashabiki wasijali. Yanga ikifanya vibaya kwa wiki mbili tu ni shida kubwa.

Advertisement

Bahati mbaya Mwakalebela amekutana na Yanga inayofanya vibaya. Lazima mchawi asakwe. Kule upande wa pili kwa wapinzani wao Simba wanafanya vizuri. Ni ngumu kusaka mchawi. Hata kina Mwina Kaguduga wanaonekana watu safi na wanaojua kuongoza timu.

Haya yanayomtokea Mwakalebela yanatokana na ubovu wa Yanga ndani ya uwanja. Hakuna kingine. Leo hatujawahi kusikia mtu anaihujumu Simba kwa sababu wana timu nzuri. Wanajua hata ukiwahujumu nje basi ndani ya uwanja Meddie Kagere na John Bocco hawawezi kukuacha salama.

Simba hawaishi maisha ya hofu. Yanga ndio ambao wanaishi maisha ya hofu. Yanga wangekuwa na uhakika na ubora wa kikosi chao, hofu ya kuhujumiwa dhidi ya Lipuli ingetoka wapi? Hakuna. Na kina Mwakalebela wangewezaje kupata kikosi bora? Kulikuwa na mambo mengi ambayo walipaswa kuyafanya kabla ya kila kitu.

Kitu cha kwanza ni kusimamia mabadiliko ya uendeshwaji wa timu yao kwa haraka. Wao walipopata Sh 500 milioni pale Diamond Jubilee wakaanza kukejeli mfumo wa mabadiliko na kudai, ‘Timu ya wananchi waendeshaji ni wananchi’.

Lakini, pia hata kama wangeweka kando mchakato wa mabadiliko bado walipaswa kutafuta njia nyingine za kuongeza kipato kikubwa klabuni. Haikuwezekana. Baadaye kina Lamine Moro walirudi makwao kwa kukosa mishahara. Baadhi ya wachezaji wa ndani pia wakakosa mishahara na kuamua kugoma.

Kampuni ya GSM iliamua kubeba majukumu ambayo sio yao na walau ilileta unafuu kwa klabu hiyo kuanzia Januari mpaka sasa. Wakati mwingine unaweza kujiuliza, bila ya GSM mambo yangekuwa vipi pale Jangwani mpaka sasa? Bakora zingetembea.

Kufikia hapo mashabiki na wanachama wamekosa imani na uongozi wao. Hata kama wana kazi nzuri wanaifanya chini chini, lakini mashabiki na wanachama wanaonekana kukosa imani na Mwenyekiti wao, Mshindo Msolla na Makamu wake, Mwakalebela.

Jaribu kufikiria tu, kama Mkurugenzi wa uendeshaji wa GSM, Injinia Hersi Said ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa kuiendesha Yanga angeenda Iringa siku chache kabla ya mechi na angekuwa mzawa wa Iringa kusingetokea shutuma hizi za kwamba, anataka kuihujumu Yanga.

Mashabiki na wanachama wa Yanga katika mioyo yao timu yao wameikabidhi kwa huyu kijana mdogo. Huku upande mwingine kwa Mwakalebela na Msolla uhusiano wao umekuwa kama samli katika kikaango chenye moto.

Uhusiano umekuwa duni na haya ndio machungu ambayo kina Mwakalebela watalazimika kuyabeba kila kukicha. Kitu kibaya zaidi ni kwamba, wanachama wetu wa siku hizi wameendekeza tabia ya kumheshimu mtu mwenye pesa tu.

Ukiwauliza watu wa Simba chanzo cha Mwenyekiti wao wa zamani, Swedi Mkwabi kujiuzulu watakwambia kwamba, alikuwa mtu sahihi sana kwao. Tatizo amezidiwa pesa nyingi na tajiri wao wa sasa, Mohammed Dewji.

Ilikuwa rahisi kwa watu wa Simba kumwambia Mkwabi awapishe bila ya kujadili kama alikuwa na matatizo ya msingi klabuni hapo. Hiki ndicho ambacho Mwakalebela atalazimika kuzoea kwa sasa. Sio yeye tu, hata Mwenyekiti Msolla atalazimika kuzoea tabia hii mpaka Yanga itakapokwenda katika mabadiliko.

Hata baadhi ya wachezaji nao wangeweza kutulia na kuiheshimu timu kama ingekuwa katika misingi imara. Usidhani kwamba Simba hakuna wachezaji wakorofi kama Bernard Morisson. Hapana, wanashindwa tu kukunjua kucha zao kwa sasa kwa sababu mifumo iko vizuri na inafanya kazi kwa kanuni na taratibu.

Advertisement