Mwadui kufufukia kwa KMC

Wednesday September 16 2020

 

MWANZA. KOCHA Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam amesema pamoja na vipigo walivyopata katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara haimaanishi timu haina uwezo, isipokuwa ni hali ya matokeo ya mpira na kwamba watabadilika na kufanya vizuri.

Timu hiyo imeanza vibaya msimu huu kwa kupoteza mechi zote mbili ikiwa ni dhidi ya Dodoma Jiji FC waliowalaza bao 1-0 na Biashara United, waliopata ushindi kama huo.

Hata hivyo Mwadui kwa misimu miwili mfululizo haijawa na matokeo mazuri kwani msimu wa 2018/19 na 2019/20 imekuwa ikiponea chupuchupu kushuka daraja na sasa hali yao msimu huu bado ni ya kusuasua.

Adam amesema hayo alipozungumza na Mwanaspoti Online amesema licha kuianza vibaya ligi, lakini si kwamba timu haina uwezo kwani vijana wake wanacheza vizuri isipokuwa wanakosa bahati ya kupata ushindi.

“Timu inacheza vizuri ishu siyo kwamba haijawa na muunganiko isipokuwa ni mambo ya mpira, hata mechi tulizocheza tumeweza kushambulia na kuzuia vizuri ila bahati haikuwa upande wetu” amesema na kuongeza

“Hata Simba yenye kikosi kilichokaa pamoja walipata sare, Barcelona huwa wanafungwa kwa hiyo hatukati tamaa na badala yake tunajiandaa dhidi ya KMC kuhakikisha tunapata ushindi” amesema kocha huyo.

Advertisement

Advertisement