Mukoko aendelea kutoa darasa Yanga

Kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe ameendelea kufumania nyavu katika nafasi anazozipata na leo Septemba 30 amefanikiwa kuipa ushindi timu yake wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM kwenye mechi ya kirafiki.

Mchezo huo umepigwa leo uliaoanza saa 1 usiku katika Uwanja wa Azam Complex ambapo Yanga ilichezesha vikosi viwili na mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza.

Bao la kwanza Mukoko alimalizia kwa kichwa kona iliyopigwa na mkali wa mipira hiyo Carlos Carlinhos dakika ya 10 na la pili dakika ya 30 beki wa KMKM alikosea kutuliza mpira, Mukoko alijitengea kisha kupiga shuti lililoenda langoni moja kwa moja.

Kiungo huyo ambaye alifunga pia kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar staili yake ya ushangiliaji kwa kuwakalisha wenzake chini na kuwa kama mwalimu imemfanya wampe jina la utani Ticha’ ikiwa na maana mwalimu.

Yanga ilicheza kwa mpira wa pasi na kushambulia kutoka pembeni mipira mingi haikuwa na faida kutokana na umakini mdogo wa washambuliaji wao kipindi cha kwanza akiwa Carlinhos na kipindi cha pili Michael Sarpong.

Kikosi cha kwanza Yanga kilichoanza kipa Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Adeyun Salehe, Makapu, Mwamnyeto, Makame, Deus Kaseke, Mukoko Tonombe, Yacouba Sogne, Carlinho, Tuisila Kisinda.

Nje ya uwanja mashabiki wa Yanga waliendeleza kuimba nyimbo za Amani wakibeba bango lililosomeka ‘Hatusapoti ngumi’ ikiwa ni ujumbe mzuri kwa tukio la mashabiki wa Simba kupigwa na kuzongwa lilitokea Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati wa mechi ya Yanga dhidi ya Mtibwa.