Muigizaji Mashaka afariki, kuzikwa kesho Kinyerezi

Muktasari:

Muigizaji Ramadhani Ditopile’Mashaka’, aliyewahi kutamba katika maigizo ya kikundi cha Sanaa cha Kaole, amefariki leo asubuhi akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Amana ambapo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa presha na kisukari.

Dar es Salaam. Muigizaji Ramadhani Ditopile ’Mashaka’, aliyefariki leo, katika hospitali ya Amana, anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kinyerezi.

Mtoto wa marehemu, Abdallah Ramadhani amesema baba yake alifikwa na umauti leo saa 2:30 asubuhi.

Mashaka alijizolea umaarufu akiwa anacheza katika kikundi cha Sanaa cha Kaole, msiba wake upo maeneo ya Ilala Bungoni na anatarajiwa kuzikwa kesho makaburi ya Tabata Kinyerezi.

Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti leo Oktoba 20, mtoto huyo anayeitwa Abdallah Ramadhani, amesema baba yake alifikwa na umauti akiwa anasubiri nesi wa kumsindikiza kwenda hospitali ya Mlongazila ambapo alipewa rufaa ya matibabu.

Akielezea zaidi, Abdalla, alisema baba yake jana majira ya saa mbili usiku alipatwa na shinikizo la damu’presha’ ghafla jambo lililowafanya wamkimbize katika hospitali ya Amana.

Walipofika huko amesema hali yake ilizidi kuwa mbaya na kulazimika kuwekewa mashine ya msaada wa kupumua.

Hata hivyo kulipokuja leo asubuhi madaktari waliamua kumpa rufaa ya kwenda hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini kwa bahati mbaya wakati wakimsubiri nesi afike maana ilikuwa wanabadilishana zamu, ndipo baba yake akafariki.

Akielezea alichokuwa akikifanya baba yake baada ya kuadimika kwenye soko la filamu, Abdalla amesema kuna kipindi baba yake aliamua kupumzika nah ii ni kutokana na kupata ugonjwa wa kupooza tangu mwaka 2013, japokuwa kuna kipindi alikuwa akichukuliwa kwenda kufundishwa baadhi ya vikundi alipopona ugonjwa huo.

Mbali na presha pia Mashaka anaelezwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.