Mugalu, Kagere watawakera zaidi, Sven adai mambo bado

HUKO mtaani mashabiki wana furaha na kutamba sana wakidai wanatamani hata kesho chama lao likutane na watani wao, Yanga kwa namna vijana wao wanavyowapa raha, lakini Kocha Mkuu wao Sven Vandenbroeck amekiri moto walionao Chris Mugalu na Meddie Kagere ni balaa.

Mugalu na Kagere kila mmoja juzi alifunga bao moja kwenye mchezo wao dhidi ya Gwambina waliowafumua mabao 3-0 ikiwa ni mara ya pili mfululizo kufanya hivyo, kwani waliwatungua pia Biashara United walipowacharaza 4-0, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ushindi huo wa pili mfululizo uliifanya Simba kuipumulia Azam FC kileleni ikitofautiana nao pointi mbili, kwani imefikisha alama 10, huku vinara hao wana 12 na mahasimu wao Yanga wakiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 10 pia kama Simba, huku KMC iliyokuwa ikiongoza tangu ligi ianze ina alama tisa katika nafasi ya nne.

Akizungumza mara baada ya mchezo wao wa Gwambina, Kocha Sven alisema kiwango na ubora unaoonyeshwa na Kagere na Mugalu ni jambo linalomfurahisha na kuamini jamaa hao watafunga sana kila atakapowapa nafasi.

Sven alisema kama kocha anafurahi kuona anaowapa nafasi hawamuangushi na kuisaidia timu kupata matokeo katika ligi inayoingia raundi ya tano wikiendi hii.

“Ukifuatilia Simba kwa muda mrefu hatujafunga bao linalotokana na mipira iliyokufa, lakini leo (juzi) dhidi ya Gwambina tumefanya hivyo mara mbili kupata mabao, ni jambo linalofurahisha, moja limefungwa na Kagere na jingine Pascal Wawa. Nimefurahishwa sana kwa hatua hii.”

Kocha huyo pia alidokeza kuwa, wachezaji wote 28 alionao kikosini wanapendana na kushirikiana, kitu ambacho kimewasaidia kila mmoja kufanya vizuri uwanjani.

“Ndani ya timu upendo na mshikamano umeongezeka kwa hali ya juu na kuthibitisha hilo angalia bao alililofunga Mugalu, ni wazi Bernard Morrison alikuwa kwenye nafasi sahihi lakini aliamua kutoa pasi ya mwisho kwa wenzake, huu ni upendo na ushirikiano mkubwa,” alisema.

BARBARA NA SEMINA

Katika hatua nyingine, vigogo wawili wa Simba waliokuwa Misri kwa ziara ya kuvuna ujuzi wa kuendesha klabu yao kisasa, Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mulamu Ng’ambi wamerejea na jana fasta wakaendesha semina kwa mastaa wa klabu hiyo sambamba na viongozi na watu wa benchi la ufundi la timu yao. Semina hiyo ilihusisha wafanyakazi wote wa Simba ilikuwa na lengo la kupeana muongozo na kuelezwa juu ya malengo ya klabu hasa kwa kile ambacho viongozi wao walijifunza Misri.