Mtibwa wawalilia mashabiki

Muktasari:

Msimu uliopita, Mtibwa Sugar ilimaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini kwa msimu huu hadi sasa iko nafasi ya 14

MWANZA. Wakati bado hawajajihakikishia kubaki Ligi Kuu, Mtibwa Sugar wamewaangukia mashabiki wao wakiwaoamba wawape sapoti kubwa katika michezo mitano iliyosalia.

Mtibwa Sugar inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 ambazo ni mbili juu ya mstari wa timu nne zinazotakiwa kushuka daraja moja kwa moja.

Akizungumza na Mwanaspoti leo, kiungo mkongwe wa Mtibwa Sugar, Abdulhalim Humud alisema uungwaji mkono wa mashabiki ni jambo kubwa linaloweza kuiokoa timu hiyo

"Tupo kwenye kipindi kigumu, nawaomba Mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono kwa kila hatua, sisi kama Wachezaji, benchi la ufundi na Viongozi kwa pamoja tumeamua kupambana kuibakiza timu Ligi Kuu" amesema kiungo huyo.

Kiungo huyo amesema kuwa wachezaji wa Mtibwa Sugar hawafurahishwi na mwenendo usioridhisha ambao wamekuwa nao msimu huu na wanajitahidi kurudi katika mstari.

"Hatuna furaha na matokeo haya. Mtibwa ni moja kati ya timu kubwa hapa nchini. Tulitamani katika mechi tano za mwisho tungekuwa tunamalizia kazi tu, lakini tumekosa bahati , tutapambana tubaki Ligi Kuu" amesema Humud.

Katika misimu iliyopita, Mtibwa Sugar ilikuwa ikifanya vyema kwenye Ligi Kuu tofauti na msimu huu ambao mambo yanaonekana kuwaendea kombo.

Msimu uliopita, Mtibwa Sugar ilimaliza ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikizidiwa pointi tano tu na KMC waliomaliza katika nafasi ya nne.

Lakini katika msimu wa 2017/2018. Mtibwa Sugar walimaliza wakiwa nafasi ya sita huku wakifanikiwa kuchukua Kombe la Shirikisho la Azam.