Mtambo wa mabao Mtibwa anakisaka kivuli cha Hazard

Monday December 10 2018

 

By Thomas Ng'itu

KIKOSI cha Mtibwa hivi sasa kinashiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) msimu uliopita.

Katika kikosi chao kuna mshambuliaji matata, Jaffary Kibaya ambaye ameonyesha umahiri katika utupiaji wa mabao baada ya kuweza kuifungia klabu hiyo mabao matatu katika ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jijini Daresalaam dhidi ya Northern Dynamo.

Mwanaspoti lilimsaka na kufanya nae mazungumzo kuhusu mipango yake ya soka ya hapo baadaye.

ALIANZIA LIGI DARAJA LA KWANZA

Kama ambavyo ilivyo kwa wachezaji wengine huanzia katika akademi ili wapate misingi ya soka, basi jambo hilo lipo mpaka kwa, Jaffary Kibaya kwasababu alianzia katika ligi za chini.

Kibaya anafunguka kwamba soka lake alianza kucheza tangu akiwa shule na baada ya hapo aliingia katika timu ya mtaani ‘Young Boys’ yenye maskani yake pale Mzumbe baada ya hapo ndio akaanza kuingia katika soka la ushindani.

“Baada ya kucheza mtaani nakumbuka msimu wa 2014 nilisajiliwa na Polisi Morogoro ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), mwaka 2015 nikasajiliwa Kurugenzi ya Mafinga nikacheza ndipo Mtibwa Sugar wakaniona,” alisema.

UGENI WA LIGI KUU WAMCHANGANYA

Baada ya kusajiliwa na Mtibwa Sugar msimu wa 2016/7, Kibaya alikiri kukutana na changamoto ya ugeni kwenye Ligi, kwa sababu ilikuwa ndio mara ya kwanza kwa upande wake.

“Maisha ya Mtibwa yalikuwa ni mageni mno kwangu kwasababu nilizoea maisha ya FDL kwa hiyo ilichukua muda mpaka kukaa sawa,” alisema.

Aliongeza suala hilo alilichukulia kama changamoto kwake kwani ndio iliyomfanya azidi kujituma kadri siku zilivyokuwa zinasonga mbele.

KILICHOMKIMBIZA MTIBWA

Msimu uliopita Kibaya aliondoka katika kikosi cha Mtibwa Sugar na kwenda kujiunga na Kagera Sugar ambao ni ndugu zake Mtibwa Sugar.

Usajili huo wengi walijua aliamua kumfata kocha wake aliyemsajili awali, Mecky Maxime ambaye aliondoka na kwenda kujiunga na Kagera Sugar, lakini mwenyewe anafunguka kwamba mkwanja ndio uliompeleka katika kambi ya Sobibo.

“Niliondoka Mtibwa kwasababu ya maslahi na nimerejea tena hapa kwasababu maslahi yao ya kunirejesha yalikuwa mazuri, ndio maana nikaamua kurejea na sio kitu kingine,” alisema.

Tangu amerejea katika kikosi cha Mtibwa amekuwa na kombinesheni nzuri na Juma Liuzio katika upande wa ushambuliaji kwani wote ni wachezaji wapambanaji.

APATA KIGUGUMIZI

Mtibwa imekuwa na kawaida ya kutoa wachezaji na kwenda kujiunga na klabu kubwa ikiwemo Simba na Yanga, hata inapofika kattika dirisha kubwa la usajili klabu hizo zinaenda kujichukulia wachezaji ambao wamefanya vizuri.

Lakini kwa Kibaya amepatwa na kigugumizi kwamba bado hajajua atatua katika kikosi kipi ikiwa amepelekewa ofa na moja ya klabu hizo zenye maskani yake katikati ya mji.

“Namuomba Mungu tu niweze kucheza kwenye timu yoyote bora ambayo ina mipango mizuri na itazidi kunifanya niwe bora zaidi ya hapa nilivyosasa,” alisema.

Aliongeza ameamua kufanya hivyo kutokana na kuhitaji kusonga mbele zaidi katika soka.

“Bado sijapata ofa kwenda nje ya nchi kwa hiyo naamini nitaendelea kubaki hapa hapa, lakini kama nikipata ofa nitaondoka,” alisema.

AWAZA KIMATAIFA

Baada kuanza vizuri kwa kufunga magoli matatu katika mchezo dhidi ya Northen Dynamo, Kibaya anafunguka kwamba hajapanga idadi kamili ya kufunga katika mashindano hayo zaidi ya kufunga kila anapopata nafasi.

“Namuomba Mungu anijaalie afya njema, halafu naamini lile ambalo Mwenyezi Mungu amenipangia kulifanya basi ndilo litakalotokea katika ufungaji,” alisema.

Aliongeza katika mashindano hayo amejikuta akitengeneza marafiki wapya kitu ambacho kwa upande wake ameona kina umuhimu katika maisha yake.

HAZARD AMUONGEZEA MZUKA

Kibaya amekuwa kati ya wachezaji anawakubali ni pamoja na staa wa Chelsea na hilo limekuwa likimfanya aonekane na utofauti mkubwa na washambuliaji wengine.

Lakini mwenyewe anafunguka kwamba mbinu hiyo ameikopi kutoka kwa Eden Hazard ambaye anasifika kwa chenga.

Anampenda mchezaji huyo namna ambavyo anacheza na mabeki wa timu pinzani, hali inayomfanya achukue baadhi ya mbinu zake.

“Hazard ni mtu ambaye anapenda kwenda mbele na kumshinikiza beki, najitahidi niwe chembe ya kopi yake kwa namna ambavyo anavyokuwa uwanjani,” alisema.

WALI SAMAKI KWAKE MZUKA

Anaonyesha kabisa kwamba anatokea Morogoro kwani anafunguka kuwa kwake ukitaka umfurahishe basi umpikie chakula aina ya wali.

“Mimi napendelea kula Wali na Samaki ukinipa na Juice hapo wala hunitoi kwani kimekuwa chakula ambacho nikikikosa kwa siku kadhaa nahisi kama nimekosa kitu cha thamani kubwa kwangu,” alissema.

Aliongeza pamoja na kupenda chakula hicho lakini matunda ni sehemu ya chakula chake na hata familia yake ameiambukiza kila wakati wamekuwa wakifata anachokihitaji hata kama anakuwa kambini lakini wao wamekuwa na mazoea hayo.

Advertisement