Msikie KDB anachosema kuhusu Messi

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO mshambuliaji wa Manchester City, Kevin De Bruyne amesema hajali kitu kama, Lionel Messi atajiunga na miamba hiyo ya Etihad mwakani.

Supastaa huyo wa Kiargentina, Messi amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Man City na alikaribia kufanya hivyo kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi wakati alipojaribu kuachana na Barcelona.

Staa huyo kwa sasa ameamua kubaki kwenye klabu yake aliyoanza nayo tangu akiwa mtoto, lakini mabosi wa Man City bado wanafuatilia kwa karibu wakiamini wanaweza kunasa saini yake kutokana na mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu.

De Bruyne, 29, alisema hajali kitu dili hilo litatokea au halitatokea la mshindi huyo mara sita wa Ballon d’Or kwenda kutua Etihad mwakani.

KDB alisema: “Wala sijali, kusema ukweli.

“Kama atakuja, kitakuwa kitu kizuri sana, kama hatakuja kuna wachezaji wengine mahiri tu nafurahia kucheza nao timu moja, itakuwa imeshindikana kwa sasa.”

Mkuu wa operesheni ya masuala ya soka kwenye klabu ya Man City, Omar Berrada alisema klabu hiyo ipo tayari kusubiri juu ya mpango huo wa kumnasa Messi, huku wakiamini atapatikana tu sokoni kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.