Mshery, golikipa kinda anayewaweka nje Kado na Nduda

MSIMU huu pale Mtibwa Sugar kwenye eneo la goli ni patashika nguo kuchanika.

Kuna makipa wanne, wawili wakiwa wakongwe kina Shaban Kado na Said Mohamed Nduda huku makinda ni Aboutwalib Msheri na Razack Ramadhan na wote wanataka kuingia kikosi cha kwanza.

Achana na Razack, huyu ni kinda na bado anakuzwa, muwazie Mshery, mzaliwa wa Tanga aliyekulia Morogoro kwa dada yake.

Kama umetazama michezo mitano iliyopita ya Mtibwa Sugar, basi utakuwa ulimuona akiokoa michomo hatari langoni kwani ndiye amedaka mechi zote hizo, huku akiwaacha nje Kado na Nduda.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka mwanzo - mwisho kuhusu maisha yake ya soka kabla, sasa na mipango ya baadaye.

Mshery alianza kucheza soka akiwa shule ya msingi kabla ya kujiunga na Kituo cha Kukuza Vipaji cha Moro Kids kilichopo mjini Morogoro, na baadaye alijiunga na kikosi cha vijana cha Mtibwa Sugar kabla ya msimu uliopita kupandishwa timu ya wakubwa.

Licha ya hapo, kipa huyo amewahi kuzitumikia timu za taifa za vijana za Serengeti Boys (2014), Ngorongoro Heroes (2018) na mwaka huo mwishoni aliitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23.

KIKOSI CHA KWANZA

Ukimuulizwa amewezaje kuwa chaguo la kwanza la Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila kwenye eneo la kipa na kuwaweka kando Nduda na Kado, Mshery anasema kuwa ni jitihada, kujituma mazoezini na nidhamu ndizo sababu zinazomfanya atue golini.

“Makipa wote ni wazuri na wana ubora wa kuanza, lakini nadhani juhudi, nidhamu na kujituma mazoezini ndizo sababu kubwa zinazofanya naaminiwa na kocha na kupewa nafasi ya kuanza,” amesema Mshery.

KUMBE TES TEGEN NDIO KIOO CHAKE

Licha ya kuwataja Aishi Manula, Shaban Kado, Juma Kaseja, Metacha Mnata na David Mapigano kama makipa bora hapa Bongo, Mshery pia anawakubali wengine wengi duniani, lakini kipa namba moja wa Barcelona, Marc Andre Tes Tegen ndiye kioo chake kwani anamfuatilia sana na kujifunza mengi kutoka kwake.

“Wengi wanadaka vizuri, lakini mtu ninayemtazama sana ni Tes Tegen wa Barcelona, yule jamaa anajua mno na ana vitu kibao vya ziada ambavyo magolikipa tunaotamani kuwa wakubwa vinatujenga na tunajifunza zaidi kupitia yeye.”

CHIRWA, BOCCO NA SARPONG NOMA

Mshery hafichi kumtaja mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa, John Bocco wa Simba na Michael Sarpong wa Yanga kuwa washambuliaji hatari zaidi anaowahofia kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

“Chirwa, Bocco na Sarporng wale jamaa ni noma, kwanza wana nguvu halafu wanalijua goli vizuri, kwa hiyo ukizubaa kidogo wanakufunga, mtu kama Bocco alivyopanda juu vile ikitokea mipira ya krosi inabidi uifuate kwa hesabu, vinginevyo utaambulia patupu... jamaa ni hatari,” anasema.

MTIBWA FRESHI

Kwa Mshery maisha ndani ya Mtibwa Sugar ni mazuri sana, na na malengo yake juu ya timu hiyo ni poa kabisa akijivunia amani na upendo vilivyopo kwa kila mchezaji ambapo wanaishi kama familia moja.

“Maisha ya hapa freshi, tunaishi kama familia na hii ipo toka kitambo, ndio maana karibu kila mchezaji aliyepita hapa bado anakuwa mwanafamilia wetu, makocha, wafanyakazi na watu wengine wanaotuzunguka wako poa sana, nahisi hiyo ndio sababu kubwa ya sisi kuishi kama familia.”

MIEZI MITANO NJE ILIMTESA

Kitu kikubwa mpaka sasa ambacho Mshery hawezi kukisahau maishani mwake ni siku aliyoumia kwenye mchezo wake wa kwanza kudaka Ligi Kuu na kumlazimu kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitano akiuguza majeraha.

“Ilikuwa ndio mechi yangu ya kwanza kudaka Ligi Kuu ikiwa ni Mtibwa dhidi ya JKT Tanzania, nakumbuka ilikuwa kwenye dakika ya 20 kuelekea 30, ulikuwa ni mpira wangu wa pili kudaka kwenye mechi hiyo ndio nikagongana na Hassan Matelema na kuumia nikatolewa nje na kuuguza jeraha hilo kwa miezi mitano,” anasema mchezaji huyo na kuonheza:

“Aisee sitakuja kusahau hii, kwani ilifika kipindi nikajikatia tamaa nikiamini nina gundu.”

NDOTO KUBWA

Mshery ameliambia Mwanaspoti kuwa ndoto zake za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ni kubwa na anaamini atazitimiza kwa kuwa umri wake bado mdogo.

“Ukiachana na kucheza timu ya Taifa, ndoto zangu nyingine ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, tena ikiwezekana kabisa iwe Ulaya kwenye ligi kubwakubwa tu, nikifeli sana iwe Uarabuni na naamini nitazifikia ndoto hizo kwa kuwa umri wangu bado mdogo na nina nguvu za kutosha kufanya hivyo, Inshaallah,” anasema.