Mourinho: Ubingwa Spurs? Mhh sijui

 LONDON, ENGLAND. JOSE Mourinho amesema hana uhakika kama kikosi chake cha Tottenham Hotspur kina akili ya kubeba mataji licha ya kuangusha kipigo cha mabao 6-1 kwa Manchester United.

Spurs ilipata ushindi wa kihistoria huko Old Trafford na kufanya wawe wamecheza mechi saba bila ya kupoteza kwenye michuano yote na kufanya timu hiyo ya Mourinho kukamatia nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Spurs haijashinda taji lolote tangu iliponyakua Kombe la Ligi mwaka 2008, huko Mourinho akikiri kwamba wachezaji wake wanahitaji kubadilika hata kimtazamo ili kubeba mataji.

ìSifahamu kama tunaweza kubeba ubingwa au la alisema Mourinho.

ìNafahamu tupambana sana kwa muda mrefu tangu nilipokuja. Msimu huu, bwana Levy na mfumo wote wa klabu umetoa nafasi kubwa ya kuboresha kikosi chao na mipango ni kushinda kila mechi.

ìLakini, ndio hivyo hatuwezi kukwepa kupoteza, tulipoteza dhidi ya Everton na tulitoka sare na Newcastle. Zaidi ya hilo, mipango yetu ni kushinda kila mechi.

“Niliwaambia wachezaji wangu, zaidi ya mara 1,000, matokeo mazuri ya Old Trafford ni ushindi. Ilikuwa akili nzuri na kiwango kilikuwa juu sana. Tukapata matokeo mazuri. Tuna pointi saba na nafasi yetu kwenye msimamo ndio hivyo.î

Mourinho alikataa kulinganisha kikosi chake cha Spurs cha sasa na kile cha Man United wakati alipokuwa akiinoa timu hiyo, ambapo alibeba Kombe la Ligi na Europa League kwa miaka miwili na nusu aliyokuwa huko Old Trafford.

“Sitaki kulinganisha timu yangu hii na ile niliyokuwa nayo Manchester United” alisema.

“Timu ile niliyokuwa nayo Man United ilibeba mataji matatu, tulishinda Europa League, kombe moja la ndani na Ngao ya Jamii.”