Moto wa Partey Arsenal wamkosha Arteta

LONDON, ENGLAND. MIKEL Arteta amemwaga sifa tele kwa kiungo wake mpya Thomas Partey kwa kile alichokifanya kwenye mchezo wake wa kwanza kuanzishwa kwenye kikosi cha Arsenal aliocheza kwa dakika zote wakati miamba hiyo ya Emirates ilipotokea nyuma na kuichapa Rapid Vienna ugenini kwenye mikikimikiki ya Europa League.

Kocha Arteta amewatisha wapinzani wao kwamba hapo Partey ndo kwanza anapasha misuli tu, mambo mengi matamu yatakuja.

Kiwango cha Partey kilionekana kuwa cha kawaida tu kwenye usiku huo wa Arsenal huko Austria, huku mabao ya David Luiz na Pierre-Emerick Aubameyang yakiwabeba na kushinda 2-1 baada ya makosa ya ya kipa Bernd Leno kuwazawadia bao la kuongoza wenyewe kwenye kipindi cha pili.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ghana alikuwa kwenye rada za Arsenal kwa muda mrefu kabla ya kutoa mkwanja kunasa huduma ya mkali wao huyo waliyemsaka kutoka Atletico Madrid katika dakika za mwisho kabisa za kufungwa kwa dirisha la usajili. Alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England alipotokea benchi dhidi ya Manchester City, lakini alikuwa moto zaidi juzi usiku alipoanzishwa kwa mara ya kwanza.

“Kwa kusema ukweli alikuwa mwamba kwelikweli, alitulia sana,” alisema Arteta.

“Nadhani aliikamatia kiungo kwenye kipindi cha pili na alifungua uwanja na kuwafanya wachezaji wa ushambuliaji kuwa huru. Alikuwa bora usiku ule na nadhani mambo matamu yatakuja zaidi.”

Arsenal ilikuwa kwenye kiwango kibovu katika kipindi cha kwanza na mambo yalionekana kuwa magumu baada ya Taxiarchis Fountas kuifungia Rapid bao.