Morrison bado pasua kichwa Yanga

Muktasari:

Hii ni mara ya pili kwa Morrison kushindwa kuonekana mazoezini tangu aliposusa kukaa kwenye benchi la timu yake baada ya kufanyiwa mabadiliko kwenye Kariakoo Derby.

MAHALI alipo winga wa Yanga, Bernard Morrison mpaka sasa bado kitendawili licha ya mapema leo Julai 14, 2020 kumpigia simu Kocha wake Luc Eymael akimuomba kurejea mazoezini na kukataliwa akitakiwa kusubiri tamko la viongozi kwanza.

Tangu Yanga ilipopoteza kwa Simba kwa kuchapwa mabao 4-1 Julai 12, 2020, Morrison aliondoka uwanjani hapo wakati mchezo bado ukiendelea kwa kile kinachoaminika kuwa ni kufanyiwa mabadiliko baada ya kuonekana hakuwa mchezoni.

Lakini, leo Jumanne Yanga imeendelea kujifua kwenye uwanja wa Chuo cha Sheria na kama kawaida Morrison hakutokea kuungana na wenzake wanaojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya vibonde walioshuka daraja, Singida United.

Mchezo huo utapigwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Yanga itakuwa ikisaka ushindi kuendelea kufukuzia kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya mabingwa mara tatu mfululizo, Simba.

Mapema leo asubuhi, Eymael alisema alipigwa simu na Morrison akiomba kurejea kuungana na wenzake lakini, akamtaka kwanza azungumze na viongozi na sio kumpigia simu yeye.

Hata hivyo, uongozi wa Yanga kupitia kwa kaimu katibu mkuu wake, Wakili Simon Patrick, imesema suala la utovu wa nidhamu uliofanywa na Morrison bado liko kwenye vikao na kwamba, muda ukifika watatoa tamko.

Wachezaji waliokuwepo kwenye mazoezi kujiandaa na mchezo huo ni Patrick Sibomana, Faruk Shikhalo, Metacha Mnata, Ramadhan Kabwili, Mrisho Ngassa, David Molinga.

Wengine ni Adeyum Saleh, Paul Godfrey, Jafar Mohamed, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Kelvin Yondani, Lamine Moro, Yikpe Gnamien, Eric Kabamba, Ally Mtoni na Haruna Niyonzima, ambaye hata hivyo hakufanya mazoezi.