Morrison atuma salamu Msimbazi

Wednesday July 8 2020

 

By Oliver Albert

Yanga imeishusha kwa muda Azam baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika leo Jumatano kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Bao la dakika 78 la Benard Morrison lilitosha kuifanya Yanga kulipa kisasi cha mzunguko wa kwanza walipofungwa na Kagera Sugar mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru.

Morrison alifunga bao hilo kwa shuti kali nje kidogo ya 18 akimalizia pasi ndefu iliyopigwa na David Molinga' Falcao.

Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 64 na kusishua kwa muda Azam yenye pointi 62 hadi nafasi ya tatu. Hata hivyo Azam itakuwa na mechi dhidi ya Mwadui itakayoanza saa 1:00 usiku leo.

Mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wa kuvutia ulishuhudia kosa kosa nyingi za wachezaji wa pande zote kutokana na uimara wa safu za ulinzi za timu zote mbili.

Mchezo huo ulianza kwa kasi  huku timu zote zikionyesha  soka safi  na dakika ya  54  Yanga ilipata faulo nje ya 18 na Benard Morrison kupiga hata hivyo beki wa Kagera  Sugar, Juma Nyoso kuokoa na kuwa kona. Morrison alipiga kona hiyo na Nchimbi  kupiga kichwa kilichotoka nje ya lango.

Advertisement

Dakika ya 72 Yanga ilipata faulo nyingine na Molinga kupiga hata hivyo iliokolewa na beki Juma Nyoso wakati Kagera ugar ilipata faulo dakika ya 77 iliyopigwa na david Luhende na kuokolewa kwa kichwa na Kelvin Yondani.

Baada ya mechi hiyo timu hiyo itarejea jijini Dar kujiandaa na nusu fainali ya Kombe la Azam Shirikisho itakayopigwa Jumapili Julai 12, 2020 katika Uwanja wa Taifa.

Advertisement