Morrison amtia hasira Dewji

Muktasari:

  • Katika mchezo wao wa mwisho ambao Simba ililala 1-0, nyota wa Yanga walipewa mzuka kwa kumwagiwa kiasi cha Sh200 milioni kama sehemu ya motisha na kweli mnyama akafa Taifa, lakini safari hii mabosi wa Msimbazi wameamua kujibu mapigo ili kumaliza tambo za Morrison
  • Simba imewekewa Sh230 milioni kama hamasa endapo itaifunga Yanga Kombe la FA zitakapokutana Julai 12

SIMBA bado wanalikumbuka lile bao la friikiki ya Bernard Morrison kwenye mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Bara na jinsi lilivyowatese mbele ya mashabiki wa Yanga, lakini sasa unaambiwa zikiwa zimesalia siku chache kabla ya timu hizo kukutana tena, bilionea wao, Mohammed ‘Mo’ Dewji ameamua kufanya yake, ili kuhakikisha Jumapili wanapindua meza kibabe mbele ya watani wao.

Simba na Yanga zitavaana kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) itakayopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuamua timu ya kucheza fainali na bilionea huyo kijana aliyepia pia Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, amewajaza upepo nyota wake kwa kuwamwagia mamilioni.

Katika mchezo wao wa mwisho ambao Simba ililala 1-0, nyota wa Yanga walipewa mzuka kwa kumwagiwa kiasi cha Sh200 milioni kama sehemu ya motisha na kweli mnyama akafa Taifa, lakini safari hii mabosi wa Msimbazi wameamua kujibu mapigo ili kumaliza tambo za Morrison.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema, Mo Dewji amepanga kuwapa donge nono nyota wake kama wataifunga Yanga na kuwatibulia kupata tiketi ya ushiriki wa michuano ya kimataifa mwakani, ikiwa ndio nafasi pekee kwa Jangwani kushiriki michuano ya CAF.

Tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tayari ipo mkononi mwa Simba iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, huku Yanga ikipambana na Azam FC na Namungo kuwania kumaliza nafasi ya pili kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mmoja wa vigogo wa Simba ameliopenyezea Mwanaspoti, bilionea huyo ametoa ahadi ya kuwapa nyota wa timu hiyo Dola za Kimarekani 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh230 milioni kwa Fedha za Kitanzania.

Kigogo huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema fedha hizo zimepangwa kupewa kwa nyota watakaoliamsha dude Uwanja wa Taifa na kuipa Simba ushindi huo muhimu wanaouhitaji ili kuwafunga mdomo watani wao wanaolitambia bao la dakika 44 la Morrison.

Kigogo huyo wa juu wa Simba, mwenye nguvu ya kufanya maamuzi aliliambia Mwanaspoti ahadi hiyo ya Sh230 milioni safari hii itakuwa tofauti katika mgao endapo wataibuka na ushindi wachezaji 11, walikuwa katika kikosi cha kwanza kila mmoja atavuta Sh20 milioni kama posho yake ambayo itakuwa jumla ya Sh220 milioni.

“Nisikilize mimi ndio nakuambia baada Dola 100,000 ukizigawanya kwa wachezaji hao 11 hapo kila mmoja atakuwa na kama mil 20 hivi na zaidi, kwa wale ambao watakuwa wameingia wakitokea benchi tutajua itakuwaje ila hiyo niliyokwambia ni kwa wale 11,” alisema kigogo huyo na kuongeza;

“Pesa hiyo ambayo tunatopa kama posho inakwenda kwa wachezaji tu kwa upande wa benchi la ufundi na wao tutajua ila huo mgao hawaingiliani,” alisema kigogo huyo.

Kiongozi huyo wa juu aliendelea kuliambia Mwanaspoti hii ni ahadi ambayo watawaeleza wachezaji hapo baadae sio sasa watakapokutana nao mara baada ya kurejea kutoka Lindi katika mchezo wao wa jana dhidi ya Namungo.

“Wachezaji wengine ambao hawatacheza tutaangalia namna gani na wao kuwafuta jasho, ila sehemu kubwa ya ahadi hazitawahusu kabisa,” alisema kiongozi huyo na kuongezea mara baada ya mchezo huo kumalizika, wataketi tena na kuangalia namna gani ya kuwapa motisha zaidi wachezaji wote kitokana na kutwaa ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo.

“Tutakaa tutaangalia tuwape nini katika kile ambacho tulikivuna kutoka kwa wdhamini wetu, kama Vodacom, Sportpesa na wengineo, si unaona mwaka jana tuliwapa bodaboda kupitia mwekezaji wetu, hivyo mwaka huu hatutawaacha patupu,” alisema.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa, aliwahi kuliambia Mwanaspoti katika kikosi chao wana utaratibu wa kutoa posho kwa wachezaji wao katika kila mechi ya mashindano iwe Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika au mashindano mengine yoyote.

Senzo alisema posho hizo huwa zinabadilika pale wanapocheza dhidi ya Yanga, Azam au timu nyingine kubwa kama ilivyo kuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na huo ni utaratibu ambao unafuata siku zote.

“Kila unapoona Simba inashinda mechi yoyote ya kimashindano ujue kuna posho ya kutosha ambayo wachezaji wetu huwa wanapata tofauti na mishahara yao na tunafanya hivyo ili kuongeza morali na motisha kwao ya kuweza kufanya vizuri zaidi na kufikia malengo yetu na hubadilika bale wanapocheza na Yanga, Azam na mashindano makubwa ya Afrika,” alisema.

Kinara wa mabao wa Simba, Meddie Kagere alisema utaratibu wa kupokea pesa kama posho kila wanaposhinda mechi ya mashindano huwa inaongeza morali na hali ya kushindana kwani huwa wanapokea mzigo wa kutosha ambao unaweza kwenda kufanyia mambo ya msingi.

“Mbali ya mshahara ambao tunapokea kwa wakati wachezaji wote lakini uongozi wetu huwa wanatupatia pesa nyingi kama posho kila tunaposhinda mechi yoyote jambo ambalo linatufanya kuwa na kiu ya kufanya hivyo kila mchezokwani mzigo unakuwa mwingi,” alisema Kagere mwenye mabao 19, mpaka sasa katika ligi.