Mbungi la fainali CAFCC kupigwa Kwa Mkapa, Mwana FA athibitisha

Muktasari:
- Itakuwa ni mara ya pili kwa Simba kuleta kombe la fainali ya mashindano ya klabu Afrika katika ardhi ya mkoa wa Dar es Salaam mara kwanza ilikuwa Novemba 1993 katika Kombe la CAF ingawa lilibebwa na timu ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Zimebaki siku 20 tu kwa wakazi wa Dar es Salaam kuliona kombe la Shirikisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 25,2025 baada ya kuhakikishiwa na Serikali kuwa mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itachezwa katika uwwnja huo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ameondoa ombwe lililokuwepo juu ya wapi ‘Mbungi’ ya fainali ya Simba na RS Berkane itachezwa akisema kipute hicho kitapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi bungeni leo Jumatatu Mei 5, 2025, Naibu Waziri huyo amesema kila kitu kimekaa sawa na tayari ameshazungumza na viongozi juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) akiwamo rais Patrice Motsepe.
“Nataka kuwahakikishia kuwa, fainali hiyo itapigwa katika uwanja wa Mkapa na hakuna namna nyingine. Tumeajili Mkandarasi kwa dharura na jana usiku nimeongea na Motsepe na kukubaliana kuwa fainali itapigwa hapo,”amesema Mwinjuma.
Simba itakutana na RS Berkane baada ya kuiondosha timu ya Stellenbosch ya Afrika ya Kusini na mechi ya kwanza itachezwa Morocco Mei 17 kabla ya kurudiana Mei 25,2025 hapa nchini.
Katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalum Nusrat Hanje ameuliza Serikali inafanya maandalizi gani kuhakikisha nchi yetu inafanya vizuri katika Mashindano ya AFCON 2027.
Akijibu swali hilo,Naibu Waziri amesema, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati miundombinu ya michezo katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Zanzibar ili kufanikisha mashindano ya AFCON, 2027 yanayotarajiwa kufanyika nchini kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda.
“Kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunasimamia malezi ya timu ya Taifa kimkakati ili kuhakikisha tunakuwa na timu bora yenye viwango vya ushindani wa kimataifa,” amesema Mwinjuma.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri,Mipango mingine ni kuboresha mikakati ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, kuandaa benchi la ufundi lililo bora, kuandaa programu za lishe, kuandaa kambi za mazoezi ya muda mrefu, kuandaa michezo ya kirafiki ya kimataifa, na kuboresha na kusimamia maslahi ya wachezaji.