Morrison: Tulieni nyie, kazi ndio kwanza imeanza

Friday January 24 2020

Morrison: Tulieni nyie, kazi ndio kwanza imeanza-Yanga Benard Morrison - Ghana-Yanga vs Singida United-MwanaspotiSoka-

 

By Thomas Ng'itu

WINGA machachari wa Yanga Benard Morrison kutoka nchini Ghana ametamba kwamba, ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya Singida ni jambo litakalokuwa na muendelezo kwa kikosi chao msimu huu.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa kwanza kwake, Morrison aligeuka kuwa nyota kutokana na uwezo wake aliouonyesha wa kumiliki mpira na pia chenga zake za maudhi zilionekana kuwa mwiba kwa mabeki wa Singida United.

Akizungumzia kuonyesha kiwango kikubwa licha ya kwamba ni mchezo wake wa kwanza alisema ni jambo la kawaida kutokana na sehemu zote kucheza soka lile lile.

“Mpira ni mchezo wa wazi na ni uleule unaochezwa sehemu yoyote. Pale unapopata nafasi inabidi uonyeshe kiwango kizuri, upate matokeo mazuri ili mashabiki, benchi la ufundi na watu wengine wafurahi,” alisema.

Aliliambia Mwanaspoti kwamba wamepoteza mechi mbili mfululizo kwa hiyo dhidi ya Singida United walikuwa wanahitaji ushindi zaidi.

“Wote tumekuja huku tukiwa na imani ya ushindi, kwahiyo ni furaha kwetu kupata ushindi huu muhimu kwetu na umerejesha furaha,” alisema.

Advertisement

Morrison alitoa pasi ya goli la pili kwa Haruna Niyonzima baada ya kuwapunguza mabeki na kutoa pasi ya nje kwa Niyonzima ambaye alipiga shuti la chinichini kwenda wavuni.

Mghana huyo amekuwa na uzoefu wa kutosha na soka la Afrika kwani kabla ya kujiunga na Yanga, amewahi kuchezea klabu za DC Motema Pembe, AS Vita Club, Orlando Pirates, Ashanti Gold na Heart of Lions.

Advertisement