Mo Salah azidi utamu Liverpool

Tuesday August 13 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND . LIVERPOOL imeanza msimu mpya wa Ligi Kuu England kwa kushusha kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Norwich City Ijumaa iliyopita na straika supastaa wa wababe hao wa Anfield, Mohamed Salah jina lake lilitokeza kwa waliotikisa nyavu usiku huo.

Kitendo hicho cha Mo Salah kufunga kimemfanya kuliweka jina lake kwenye kitabu cha historia ya kipekee kwenye timu hiyo.

Baada ya Grant Hanley kujifunga kuifanya Liverpool kuongoza, mshindi mara mbili mfululizo wa Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England, Mo Salah alifunga bao la pili na kuwafanya wakali hao wa Kocha Jurgen Klopp kutulia na kuibuka na ushindi wao mnono.

Kwa msimu wa tatu mfululizo, Mo Salah amekuwa akifunga bao kwenye mechi za kwanza za Liverpool kwenye Ligi Kuu England na sasa amefikisha mabao 72 tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea AS Roma mwaka 2017.

Tangu Liverpool ilipoanzishwa mwaka 1892, wachezaji 452 wameifungia timu hiyo, lakini idadi hiyo ya mabao aliyofunga Mo Salah sasa inamwingiza kwenye mastaa 30 vinara wa mabao wa muda wote katika kikosi hicho, kwa mujibu wa LFC History.

Kitu kinachovutia ni kwamba huu ndio kwanza msimu wa tatu kwa Salah na amecheza mechi 106 tu, akiendelea kubaki hapo kwa muda mrefu atavunja rekodi nyingi zaidi. Hata hivyo, bado ana safari ndefu kuvunja rekodi ya staa Ian Rush, aliyefunga mabao 346 katika kikosi hicho.

Advertisement

Advertisement