Mo Rashid kimeeleweka KMC

Muktasari:

  • Mo Rashid aliliambia Mwanaspoti kwamba tayari amemalizana na KMC, kilichobakia ni kusubiri timu irejee Dar es Salaam, ili kocha wake mpya, Etienne Ndayiragije aanze kumpangia majukumu.

MSHAMBULIAJI wa Simba, Mohamed Rashid ‘Mo Rashid’ atajiunga kwa mkopo na timu ya KMC ikirejea jijini Dar es Salaam kutoka Shinyanga ilikokwenda kucheza na Mwadui FC jana Jumatatu.

Mo Rashid aliliambia Mwanaspoti kwamba tayari amemalizana na KMC, kilichobakia ni kusubiri timu irejee Dar es Salaam, ili kocha wake mpya, Etienne Ndayiragije aanze kumpangia majukumu.

Pia, Mo ambaye atakuwa na klabu hiyo kwa mkopo wa miezi sita, alitoa sababu ya kuichagua KMC na sio Prisons, Coastal Union, Mwadui FC na Singida United ambazo zilipeleka ofa mezani kwa Simba.

“Nimeamua kutumikia KMC kwa muda uliobakia kumaliza msimu huu kutokana na kukidhi vigezo nilivyokuwa navitaka, lakini si kama timu nyingine sikutaka kufanya nazo kazi.

“Nimekubali kutolewa kwa mkopo na Simba ili niweze kupata nafasi ndani ya kikosi cha kwanza. Naamini nitafunga sana tu mbali na kwamba nilikuwa nacheza dakika chache, lakini nilikuwa nafanya mazoezi kama mchezaji anayetegemewa na Kocha Patrick Aussems,” alisema. Alifichua tangu ajiunge na Simba amejifunza ufundi mwingi kutoka kwa kocha na wachezaji wenzake.