Mo Rashid anogewa ang'ang'ania KMC

Muktasari:

CAF ilibadilisha kanuni ya kuingiza timu nne katika Mashindano ya CAF kwa kuingiza timu mbili katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mohammed Rashid ‘Mo Rashid’ anayeichezea kwa mkopo KMC amenogewa na maisha ya Kino Boys kiasi cha kuanza kufikilia kusalia katika kikosi hiko.

Mo alisajiliwa na Simba akitokea Prisons, lakini alishindwa kupata namba katika kikosi cha Mbelgiji Aussems na kutolewa kwa mkopo katika dirisha dogo msimu huu.

Mo alisema baada ya msimu kumalizika hivi sasa anaangalia namna ambavyo atapata nafasi zaidi ya kucheza katika kikosi cha KMC kilichofanikiwa kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

"Mimi binafsi nataka kuendelea kusalia hapa nipate nafasi ya kucheza zaidi, najua nahitajika kurudi Simba, lakini nitazungumza na viongozi wangu pamoja na mwalimu tujue inakuaje," alisema mshambuliaji huyo.

Hata kama Mo akiendelea kusalia katika kikosi cha KMC atashiriki mashindano ya kimataifa baada ya timu hiyo kuingizwa kutokana na kushiriki nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.

CAF ilibadilisha kanuni ya kuingiza timu nne katika Mashindano ya CAF kwa kuingiza timu mbili katika klabu bingwa na Shirikisho Afrika mbili.