Mo Dewji,Mkwabi mambo freshi

Tuesday July 16 2019

 

By Thobias Sebastian

KAMA kuna watu waliokuwa wakiamini Simba itayumba, pole yao kwani ule mzozo uliowachanganya mashabiki wa klabu hiyo, umekwisha kiulaini na sasa mabosi wa klabu hiyo ni kazi kwa kwenda mbele ili kuifanya klabu hiyo kujitofautisha na nyingine.

Kwa wiki moja na ushei, hali klabuni hapo haikuwa shwari kutokana na kilichoelezwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba ambaye ndiye mwekezaji, Bilionea Mohammed Dewji na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi kutoelewana.

Dewji alikuwa akitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kuandika mafumbo yakiambatana na picha, kabla ya kuja kubainika alikuwa akipanga kujiuzulu kwa sababu kuu tano kwa kuamini Mkwabi anamkwamisha Msimbazi, lakini mambo yameisha.

Bodi ya wakurugenzi wa Simba juzi Jumamosi ilikutana na kujadili mambo kadhaa ikiwemo kupata suluhisho ya Mo Dewji na Mkwabi na kila mmoja kiroho safi ameafiki kuzika tofauti zote za nyuma baada ya kuelewana.

Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kuwa ajenda zilizokuwepo ni kupitia kanuni zilizowekwa kwa ajili ya wachezaji na benchi la ufundi (Code of Conduct), malengo ambayo wamejiwekea msimu ujao, kutathimi usajili na kusuluhisha suala la Mo Dewji na Mkwabi ambalo lilichukua muda mrefu kuliko ajenda zote.

Mtoa taarifa huyo alisema Mo Dewji na Mkwabi walizungumza madukuku yao na baada ya hapo walipatana na kila mmoja kuahidi kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Advertisement

“Tulimaliza mkutano kila mtu akiwa na amani ya kutimiza majukumu yake kwa nguvu vilivyo, lakini cha kushangaza usiku Mo Dewji alijitoa katika baadhi ya makundi ya muhimu ya WhatsApp,” alisema mtoa taarifa huyo (Jina lake tunalo).

YACHUKUA JEMBE

Miongoni mwa yalijadiliwa katika kikao hicho ni kuhusu ajira mpya. Simba imeshapitia nafasi ya Mhasibu Mkuu, Ofisa wa Wanachama na Mtendaji Mkuu anayeenda kuchukua nafasi ya Crescentius Magori.

Licha ya Mwanaspoti kushindwa kupenyezewa majina ya waliomba nafasi hizo, limenusa taarifa kwenye Idara ya Habari, inayosaka Ofisa Habari mmoja ya walioomba ni Mwandishi wa zamani wa Mwanaspoti, linalozalishwa na Mwananchi Communications Ltd, Gift Macha anayetajwa kupewa nafasi kubwa kupewa cheo hicho.

Nafasi hiyo inashikiliwa na Haji Manara na Macha ana uwezekano mkubwa kuipata.

Advertisement