Mkwasa kazi anayo kwa Ndanda

Muktasari:

Yanga wamekuwa wababe wa Ndanda wanapokuwa Dar es Salaam, rekodi zikionyesha katika michezo sita ukiwemo ule wa sare ya mabao 2-2 ambao Ndanda waliomba uchezwe Dar pamoja na kuwa walikuwa wenyeji, pia wameshinda mara tatu na kutoka sare mara tatu.

CHARLES Boniface Mkwasa, aliyebebeshwa kwa muda mikoba ya Mwinyi Zahera leo Ijumaa ana kibarua kizito kwenye Uwanja wa Nagwanda Sijaona mjini Mtwara wakati atakapoiongoza Yanga kuikabili Ndanda FC katika Ligi Kuu Bara.

Hii itakuwa ni mechi ya tano kwa Yanga na ya kwanza tangu Zahera atupiwe virago na Mkwasa kukabidhiwa kwa muda wa wiki mbili, wakati kocha mkuu mpya akisakwa.

Yanga wenye pointi saba katika wakiwa nafasi ya 17, watawakabili Ndanda ambao wamekuwa na rekodi nzuri hasa wanapocheza nao uwanja wao wa nyumbani.

Vilevile itakuwa ni mara ya 11 ndani ya misimu sita kwa Yanga na Ndanda kukutana Ligi Kuu tangu 2014/15 ambapo Ndanda walishiriki kwa mara ya kwanza. Yanga wameibuka na ushindi mara moja kwenye uwanja wa Nangwanda huku wakipoteza mara moja na kutoka sare mara mbili.

Yanga wamekuwa wababe wa Ndanda wanapokuwa Dar es Salaam, rekodi zikionyesha katika michezo sita ukiwemo ule wa sare ya mabao 2-2 ambao Ndanda waliomba uchezwe Dar pamoja na kuwa walikuwa wenyeji, pia wameshinda mara tatu na kutoka sare mara tatu.

Mara ya kwanza kwa Yanga kucheza na Ndanda, ilikuwa 2014/15 walipokutana Yanga wakiwa wenyeji walilazimishwa suluhu Februari Mosi, 2015 kabla ya kulala 1-0 mjini Mtwara Mei 9, ambapo Yanga pia walibeba ubingwa kwa alama 55 na Ndanda walimaliza nafasi ya tisa na pointi 31. Msimu wa pili kukutana timu hizo zilimaliza katika nafasi hizohizo tofauti ikiwa ni pointi, Yanga wakitwaa ubingwa tena na pointi 73, Ndanda wakamaliza nafasi ya tisa na pointi 35.

Katika msimu huo wa 2015/16, Yanga walivunja mwiko kwa kushinda dhidi ya Ndanda wakiibuka na ushindi jijini Dar kwa bao 1-0, Januari 17, 2016, na mchezo wa marudiano uliokuwa upigwe Nangwanda Ndanda waliuhamishia Dar ili kuvuna mapato na matokeo kuwa 2-2.

Katika msimu wa tatu wa Ndanda, Mei 15, 2016, Yanga walibeba tena ubingwa wakimaliza na pointi 68, lakini hali ya Ndanda ikaonekana tete kutokana na kunusurika kushuka daraja wakimaliza nafasi ya 13 kati ya timu 16 na pointi zao 33. Msimu huo wa 2016/17, Ndanda waliibana nyumbani Yanga wakitoka suluhu Septemba 7, 2016 lakini wakaja kukubali kipigo Dar kwa kuchapwa mabao 4-0, Desemba 28, 2016.

Msimu wa 2017/18, Yanga waliifunga Ndanda jijini Dar bao 1-0, Septemba 23, 2017 na kushinda pia Mtwara kwa mara ya kwanza kwa mabao 2-1, Februari 28,2018, japo Yanga iliutema ubingwa kwa Simba kwani Yanga ilimaliza ya tatu nyuma ya Azam waliokuwa nafasi ya pili.

Katika msimu uliopita wa 2018/19 timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare nyumbani na ugenini mechi zilizopigwa Novemba 4, 2018 na Aprili 4, 2019.

MAKOCHA

“Uzuri nimeikuta timu ikiwa imetoka katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa, kuna mambo madogo ambayo tumeelekezana, kikubwa mashabiki wajitokeze kutusapoti, sina shaka ya uwezo wa wachezaji wa Yanga,” alisema kaimu kocha, Mkwasa.

Kocha wa Ndanda, Malale Hamis alisema, “Tunaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu kubwa, lakini hilo halituzuii kupigania pointi tatu, timu yangu ipo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo.” Michezo mingine leo Azam FC wataikaribisha Biashara United huku KMC wakicheza na Kagera Sugar.