Mkwasa: Nimevumilia mengi kwa Eymael

Muktasari:

Mkwasa amesema Eymael hakuwahi kusikiliza ushauri wa wasaidizi wake hadi timu ilipokwama ndipo alipowasikiliza

Dar es Salaam. Kocha Charles Mkwasa ametoboa namna walivyofanya kazi na aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael kabla ya kutimuliwa juzi kutokana na matamshi ya kibaguzi.

Mkwasa, kocha msaidizi wa Yanga alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana akisema alishindwa kuzungumza awali kwa sababu angeonekana kama anamchongea kocha huyo raia wa Ubelgiji.

“Tulijaribu kumsaidia, lakini hasaidiki,” alisema Mkwasa aliyewahi pia kuwa mchezaji na katibu mkuu wa Yanga kwa nyakati tofauti.

Alisema Eymael hakuwahi kusikiliza ushauri wa wasaidizi wake hadi timu ilipokwama ndipo alipowasikiliza.

“Mambo mengi yalikuwa hayaendi, tulivumilia vingi, ilifikia mahali timu ilikuwa inapoteza mwelekeo, lakini tunashindwa kusema sababu tungeonekana tunamchongea.

“Lakini mwisho wa siku ukweli umeonekana,” alisema Mkwasa akisisitiza kuwa kocha huyo alinusurika mara kadhaa kupewa kadi nyekundu akiwa kwenye benchi kutokana na matamshi yake.

“Tulikuwa tukiwaomba waamuzi watusamehe sisi kutokana na matamshi yake kwao, lakini kama ni kadi nyekundu angeshapewa siku nyingi.”

Hata hivyo, kocha wa makipa wa Yanga, Peter Manyika ambaye kuna tetesi alitaka kuzichapa na Eymael alisema hayupo katika nafasi ya kuzungumzia sakata hilo kwa undani.

“Uongozi unafahamu kila kitu kuhusu tulivyoishi na kocha mkuu (Eymael), hivyo wao ndiyo wataeleza ipasavyo kwani muda mwingi wakati tunatofautiana naye (Eymael) Bumbuli (ofisa habari wa klabu) alikuwepo,” alisema.

Bumbuli alipoulizwa alisema klabu yao sasa inasonga mbele na imeachana na habari za Eymael ambaye alidai alikuja kuinoa Yanga kwa bahati mbaya.

Naye beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul alisema kuondoka kwa Eymael kumewaumiza kama wachezaji, lakini aliuomba uongozi kuwatafutia kocha mwenye viwango na wachezaji wa maana ili waweze kuendana na muda uliopo.

Juzi, Yanga ilitangaza kumtimua kocha wao Eymael kutokana na sauti iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiashiria ubaguzi kwa mashabiki na kauli zisizo za kiungwana na kiuanamichezo zilizotolewa na kocha huyo.

Kocha huyo alitimuliwa wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imemalizika, huku wachezaji wa Yanga wakipewa wiki mbili za mapumziko kabla ya kurejea mazoezini.

Abdul alisema kuwa anaamini kutokana na muda mfupi uliopo itakuwa vigumu kwao kuelewana haraka na kocha mpya, hivyo uongozi unapaswa kuwatafutia kocha mwenye viwango vya juu ambaye hatakuwa na mambo mengi.

“Tumesikitika kuondoka kwa Eymael, kwani kama wachezaji tuliishi naye vizuri na kama unavyojua hata katika familia mkizoeana mmoja anapoondoka inakuwa ni huzuni,” alisema.

“Hata hivyo maisha lazima yaendelee na naamini uongozi uko kwenye mchakato wa kumtafuta kocha mpya, maana ukiangalia muda ni mdogo kabla ya kuanza msimu mwingine wa ligi.

“Kazi itakuwepo kwani hakuna kitu kigumu kama kubadilishiwa kocha halafu ni muda mfupi kabla ya ligi, inakuwa ngumu kuelewana haraka, nikimaanisha kushika falsafa zake. Ndio maana timu inatakiwa kuwa na kocha karibu mwaka mzima ndio inakuwa sawa na kucheza kwa ubora wake.”

Aliongeza kuwa: “Nimesikia Yanga inakwenda kufanyiwa marekebisho ikiwa na maana wachezaji wengi wataondoka. Sasa ikiwa wengi wataondoka ina maana watakuja wengi wapya ambao wataungana na wale wachache watakaobaki kikosini halafu wanakutana na kocha mpya, hapo ugumu sasa ndipo utakapokuwepo.

“Muhimu ninachowaomba viongozi watafute kocha mwenye kiwango kikubwa ambaye tutamuelewa kwa muda mfupi na pia wasajili wachezaji wenye viwango ili timu isiyumbe kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Naamini kama uongozi utafanya, ikiwemo kuongeza wachezaji wenye ubora watakaoshirikiana na wale watakaobaki basi msimu ujao unaweza kuwa mzuri kwetu.”

Yanga ilimfuta kazi Eymael juzi na kumtaka kuondoka nchini haraka kwa kutoa kauli ya kibaguzi, ingawa kocha huyo alikaririwa na gazeti hili jana akisema sio mbaguzi wa rangi.