Mkina awatuliza Pamba SC

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkina alisema mabao hayo yamempa nguvu na moyo wa kujiamini zaidi, hivyo katika mechi zijazo za Ligi Daraja la Kwanza, atafanya kila jitihada afunge kila mchezo ili aendeleze furaha yake na mashabiki wa Pamba.

JUMAMOSI iliyopita straika wa Pamba, Shija Mkina aliifungia timu yake mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Green Warriors ikiwa ni mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza katika Kundi B kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini hapa.

Lakini baada ya kufunga mabao hayo kwa mara yake ya kwanza katika mechi nane ambazo Pamba imecheza, Mkina amewataka mashabiki wao watulize mzuka kwani mambo mazuri zaidi yanakuja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkina alisema mabao hayo yamempa nguvu na moyo wa kujiamini zaidi, hivyo katika mechi zijazo za Ligi Daraja la Kwanza, atafanya kila jitihada afunge kila mchezo ili aendeleze furaha yake na mashabiki wa Pamba.

“Mechi Saba za mwanzo sikupata bahati ya kufunga, jambo hilo lilikuwa linaniumiza kichwa sana, lakini nimepata furaha baada ya kufunga haya mawili, nawaahidi mashabiki wetu nitaendelea kupambana ili nifunge kila mchezo,” alisema Mkina.

Aliongeza kazi yake kubwa uwanjani ni kufunga na kuisaidia timu yake kuibuka na pointi tatu katika kila mchezo, lakini suala la kutikisa nyavu lilikuwa gumu hapo mwanzo hii ni kwasababu ushindani umekuwa mkali sana msimu huu.