Mkataba wa Morrison na Simba siri yavuja

Sunday October 04 2020
mkataba bm pic

SAKATA la mkataba wa winga Mghana Bernard Morrison na klabu yake ya Simba limeingia katika sura nyingine baada ya kuwepo na taarifa mkataba huo ulivujishwa na mmoja wa maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuwapelekea Yanga.

Aidha Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF, baada ya kusikia maneno mengi juu ya sakata hilo imeamua kuitana jijini Dar es Salaam, Jumatatu ya wiki ijayo ili kulijadili na kulitolea maamuzi, huku Mwenyekiti wake, Elias Mwanjala akisisitiza ukweli wa kila kitu juu ya mkataba huo utafahamika tu.

Katikati ya wiki hii, uongozi wa Yanga ulilalamika juu ya TFF kuupokea mkataba wenye mapungufu mengi ulioonyeshwa umesainiwa na Morrison pekee na kusajiliwa kwenye TMS na kutoka leseni yake ya kucheza ligi wakati mkataba wao wa miaka miwili wa halali waliukataa wakidai una mapungufu.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyosikiliza kesi ya Morrison dhidi ya Yanga juu ya mkataba mpya wa miaka miwili ulimtangaza winga huyo kuwa mchezaji huru kwa madai ya mkataba huo kuwa na mapungufu na kumruhusu ajiunge na Simba, licha ya kumkatia rufaa.

Ndipo juzi kati wakaibuka na kudai mkataba uliomhalalisha Morrison Simba ulikuwa na dosari nyingi, huku baadhi ya viongozi wa Simba wakihoji watani wao wameupata wapi, hata hivyo, Mwanaspoti limedokewa siri hiyo ilivujishwa na watu waliopo ndani ya TFF kuwapa silaha Yanga.

Mmoja ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba (jina tunalo) alikiri uhalali wa mkataba uliovujishwa na Yanga wakiulalamikia kuwa na saini moja tu na kudai wa kulaumiwa ni TFF walioupokea ukiwa na mapungufu bila kuwaambia lolote, japo Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ akidai Yanga wameingia chaka kwani mkataba waliouonyesha ni feki.

Advertisement

Mjumbe huyo alisema upande wao na Morrison hakuna aliyelalamika juu ya mapungufu hayo ambayo wanaona ni rahisi kuyarekebisha huku akidai lilikuwa jukumu la TFF kuwataka kurekebisha sehemu zenye mapungufu na kusisitiza;

“Tunafahamu kinachoendelea na tumewaagiza viongozi wa juu kushughulikia hilo na mchezo mzima ulivyochezwa pale TFF tunaufahamu, ingawa sio tatizo kubwa kwetu kwani ni jambo la kufanyia marekebisho tu mkataba.”

Mjumbe huyo aliongeza; “Mkataba kama pande zote mbili hakuna aliyelalamika (Simba na Morrison) basi linakuwa jepesi kwani haya ni makubaliano yetu na si mwingine. Tunasubiri TFF watuelekeze nini cha kufanya maana ni suala la marekebisho tu na kuurudisha. Ni kweli hata Fifa itaonyesha kwa mara ya mwisho Morrison alikuwa Yanga maana usajili unapotumwa unaonyesha wapi mcheza ametoka kwenye zile ICT (Uhamisho wa Kimataifa).

Aliwatuliza mshabiki wa Simba kwa kuwaambia wasiwe na wasiwasi wala kuchanganyikiwa kwani suala hilo litakwisha nawanasubiri TFF iwape muongozo juu ya mapungufu hayo.

Advertisement