Mkapa awaliza Bongo Movie

Saturday July 25 2020

 

By CLEZENCIA TRYPHONE

KUFUATIA kifo cha Rais Mstaafu wa Jamuhiri ya Muungano Tanzania, Benjamini Mkapa wasanii mbalimbali wakiwemo Bongo Movie ambao wameelezea hisia zao kwenye mitandao yao ya kijamii.

Hayati Mkapa amefariki usiku wa kuamkia leo Ijumaa katika akiwa anapatiwa matibabu hospitalini jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa wasanii waliotumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuandika maneno ya kuomboleza ni msanii wa vichekesho Lucas Mhavile 'Joti' aliyeandika hivi;

"Hakika Mwenyezi Mungu ndie mwenye kujua muda, siku, saa, Leo muda umefika kwake aliyekuwa Rais wetu wa awamu ya tatu, Benjamini William Mkapa. RIP Mzee Wetu.MwenyeziMungu ametekeleza wajibu wake na wajibu huu lazima kila mwanadamu umkute ili neno lake Bwana litimie.

Joti ameongeza, "Nafasi pekee tuliyoibakiza hapa duniani ni Ibada tu, hakika hayo mengine ni mapito tu..Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi Amina,".

Naye Gabo Zigamba ameandika ''Busara za Taifa zimemfuata baba wa Taifa, nitakukumbuka daima, maneno yako mchakato, mkukuta, mkurabita, upembuzi yakinifu na utandawazi,''

Advertisement

''Kiongozi wetu, mweledi wa kiswahili, Rais uliyeheshimika Duniani, Barani, Nchini , Mtaani, ukitoa hotuba lazima imakiniwe, ukitoa ushauri lazima upokelewe, ukituma neno jipya lazima liigwe, Mungu akusamehe ulipoteleza ukiwa Duniani,''

Jacqline Wolper naye ameandika kwamba "Rest in Peace shua, poleni Watanzania ndugu jamaa na wanasiasa wote,"

Naye Halima Yahya ameweka picha ya hayati Mkapa na kuandika katika ukurasa wake "Pumzika kwa amani baba yetu, mbele yako nyuma yetu,"

Kwa upande wa Jacob Steven 'JB' katika kuonyesha kuomboleza kifo hicho kupitia ukurasa wake wa Instagramu ameandika ''Pumzika kwa amani mzee wetu, poleni Watanzania wenzangu poleni familia,''

Huku Dr Chen akiweka picha akiwa na Mkapa katika ukurasa wake na kuandika "Mh Rais Mstaafu Mzee wetu Mkapa tulipenda tuwe nawe kwenye kampeni za mwaka huu ila Mungu amekupenda zaidi, pumzika kwa amani mzee wetu,''

Advertisement