Mikasa ya Duchu

SIMBA imebadili historia ya beki wao, David Kameta ‘Duchu’ (19), ambaye amepitia mazito, yanayomfanya awe nidhamu, mpole, bidii katika kazi zake na ubinadamu anapoona mtu mwingine anapitia magumu.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Duchu, anafunguka mapito yake mpaka anasajiliwa Simba, anayokiri angalau imempa unafuu wa baadhi ya mambo katika maisha yake.

Ingawa historia yake inaweza ikashabihiana na mastaa wanaotikisa ulaya kama Cristiano Ronaldo ambaye ni kioo cha wengi kutamani kufikia mafanikio aliyonayo kiuchumi, kujulikana na uwezo, ila nyuma ya hayo yote, alitokea familia ya kimaskini.

Wakati akiwa mdogo Ronaldo ambaye kwa sasa anatamba akiwa na miamba ya soka la Italia, Juventus alikuwa akilala chumba kimoja na dada zake ambao alizaliwa nao familia moja yote hiyo ilitokana na umaskini wa familia yake.

Wakati Duchu anasimulia baadhi ya mapito yake uso wake ulimjaa machozi, huku akisisitiza hapendelei kuongea ongea badala yake anapenda kufanya kazi kwa bidii, anazoamini zitabadili mwanzo mnyonge nakuwa shujaa wa badae.

“Sipendi kuongelea baadhi ya mambo ambayo yamewahi kuniumiza moyo, nayachukulia kama chachu yakujituma kwa bidii ili nije niishi uhalisia wa ndoto zangu, nalazimika kusema haya kwasababu ya maswali yako,”anasema.

UNYAMA WA MJOMBA WAKE

Duchu anasimulia mkasa ulioacha alama ya maumivu moyoni mwake, anasema mama yake, Kissa Mwaikole aliachana na baba yake muda mrefu, hivyo wakawa wanaishi kwa babu yao (mzaa mama yake).

Anasema babu yake Mwaikole alimpa nyumba ya urithi, ambayo walianza kuishi yeye, mama na dada zake wawili kwa kuwa wamezaliwa watatu, lakini kitu ambacho alikuja kuwafanyia mjomba wake, kiliwatoa machozi na kuwapa aibu mbele ya majirani zao.

“Tulikaa kwenye ile nyumba takribani miezi kama 10 hivi, mjomba kaka yake na mama, aliuza nyumba bila kutuambia wakati babu alinipa urithi mimi, tukaondoka kwa aibu kwenda kupanga na wakati huo maisha yetu yalikuwa duni sana,” anasema Duchu na anaongeza kuwa.

“Siku ambayo walionunua nyumba wanakuja kuishi, nilimuona mama yangu akitoa chozi kwa uchungu, akituangalia mimi na dada zangu, majira kama unavyojua wapo waliotucheka, wengine wakatuonea huruma, tukio lile liliniumiza sana, nilihisi moyo wangu kama umemwagiwa barafu, ingawa nilijikaza kiume ili nisimuumize mama, kwani mimi ni wa mwisho halafu wa kiume pekee kuzaliwa,”anasema Duchu.

Anasema wakakusanya vilago vyao, kisha wakatafuta nyumba wakapanga na kuendelea na maisha yao, jambo analofichua lilichangia yeye kujituma kwa bidii katika soka, ili aweze kumfuta machozi mama yake ambaye aliwahangaikia toka wadogo, kuhakikisha wanakula, wanavaa na kwenda shule.

“Tukio hilo ni miaka mitatu nyuma, nakumbuka nilikuwa na umri wa miaka 16 kama si 15 nilikuwa katika kituo cha soka cha Foisa kipo jijini Mbeya, nikakazana kucheza ndipo Mungu amefungua milango leo hii nipo Simba, hivyo watu wasione nipo nipo tu, natamani kufika mbali,”anasema Duchu.

AMPA KICHEKO MAMA YAKE

Simba imemsajili Duchu kutoka Lipuli iliyoshuka daraja msimu uliopita, anakiri ni hatua kubwa katika maisha yake pia ni jambo lililomtoa machozi ya furaha mama yake Kissa, aliyemuambia maneno mazito yanayoishi akilini mwake.

“Wakati namwambia mama viongozi wa Simba wanafanya mazungumzo na mimi, akaniangalia, akatabasamu kisha akatoa jozi na kuinamisha kichwa chake kumshukuru Mungu, badae akaniombea na kuanza kuniambia maneno haya,”anasema Duchu na anaendelea kusimulia.

“Aliniambia mwanangu nakutazama kama baba yangu, rafiki yangu, mtoto wangu, nenda kafanye kazi nakujitenga na dunia, nakutegemea ukiyumba utakuwa umeniyumbisha, niliumia sana ingawa sura yangu ilikuwa imejaa tabasamu lakumpa moyo mama, lakini moyoni nikaweka dhamira kwamba nikipata nitaitumia kwa umakini wa hali ya juu, ili nizidi kusonga mbele,” anasema Duchu na anaongeza kuwa.

“Ndio maana sina mambo mengi zaidi yakupambana kuhakikisha nafika mbali, nashukuru Mungu njia za mafanikio yangu zimeanza kufunguka, Lipuli ulikuwa msimu wangu wa kwanza na sasa nipo Simba, nikifanya bidii najua nitafika mbali zaidi ya hapa,”anasema.

SIMBA ILIKUWA NDOTO YAKE

Duchu baada ya kutoka kwenye kituo cha soka cha Foisa, alijiunga na Prisons (Under-20) badae akahamia Mbeya City (Under -20), anasema Simba ilikuwa ikienda kucheza na timu hizo, alikuwa anatamani siku moja aje kuvaa uzi mwekundu na sasa ndoto yake inaishi.

“Nilikuwa natamani kuichezea Simba, hii ndoto imetimia zimebakia mbili, kucheza timu ya Taifa Stars na nje ya nchi kama ilivyo kwa kaka zangu, Mbwana Samatta na Simon Msuva ambao wana mafanikio kwa kizazi cha sasa, hivyo ni kujituma na kutokukata tamaa,”anasema.

NYONI, BOCCO NA KAPOMBE

Nje na beki Shomary Kapombe ambaye anamtazama kama kioo chakucheza namba yake, anamtaja Erasto Nyoni na John Bocco, kwamba niwachezaji alioanza kuwaona tangu akiwa mdogo, lakini bado wapo kwenye kiwango cha juu, jambo analoona limewashinda chipukizi wengi.

“Ni wachezaji ambao wanafaa kuigwa kwa namna ambavyo wametunza miili yao, nimejiona ni mwenye bahati kukutana nao Simba, ingawa sijawazoea kihivyo ila naamini ipo siku nitakaa nao, ili kujua wamewezaje kujitunza mpaka sasa,” anasema Duchu na anaongeza kuwa.

“Nina malengo yakufika mbali ndio maana napenda kujifunza kwa wale ambao wana vitu vyakunifikisha katika ndoto zangu, ndio maana nimemtaja Nyoni na Bocco ambao nimewaona kitambo na bado wapo vizuri, lakini pia wanazingatia sana mazoezi,”anasema Duchu.

SIMBA IMEMPA HATUA HII

Ingawa hataki kuweka wazi ni vitu gani amevifanya baada ya kuvuta mkwanja wake wa usajili Simba, jambo kubwa anasema kwasasa mama yake mzazi anaishi kwa amani tofauti na mwanzo, jambo linalompa furaha na bidii ya kazi.

“Nasisitiza sipendi kuongea sana, ila vitu vingi vimebadilika kwa muda mfupi, tayari mama anakaa sehemu aliyo na amani nayo, naamini taratibu naanza kumfuta machozi ambayo aliyatoa mbele yetu baada yakuona maisha yake magumu na anatamani kutufanyia kila kitu ila alikuwa anashindwa,”anasema.

Nje na maisha kubadilika kiuchumi, anazungumzia kuhusiana na kazi yake kwamba ameanza kujifunza mbinu za kiufundi kwa kupata mazoezi yanayomjengea ufiti na pia kuishi maisha anayotakiwa mchezaji anayejitambua na mwenye malengo ya kufika mbali.

“Japokuwa sijaanza kupangwa kwenye kikosi cha kwanza, kutokana na ubora alionao kaka yangu Kapombe, lakini napata mwanga na uvumilivu kwamba ipo siku na mimi nitakuwa tegemeo ndani ya timu na kulitumikia taifa langu la Tanzania,”anasema.

ANACHOAMBIWA NA KAPOMBE

Anasema jambo la kwanza baada yakujiunga na Simba, alikwenda kumfungukia Kapombe jinsi anavyomkubali na kujua siri yakudumu kwenye kiwango anachokionyesha kinachofanya ajihakikishie namba kwenye kikosi cha kwanza ndani ya timu na Taifa Stars.

“Kwanza nilidhani labda angeniletea dharau, ajabu akanikalisha chini nakuanza kunisaidia kufanya mazoezi ya aina gani yanaweza yanakifanya niwe fiti, pumzi na stamina, pia nikicheza mechi za kirafiki ananiita nakuniambia hapa ulitakiwa ufanye hiki na pale umepatia,”anasema na kuongeza kuwa.

“Naamini nitajifunza vitu vingi kutoka kwake kwani ni mchezaji ambaye anapenda mwingine afanikiwa pia anapenda ushindani anaoamini utaendelea kumfanya awe bora, hivyo nina nafasi yakuja kuwa beki muhimu kadri muda unavyokwenda,”anasema.

NAFASI YAKE YA KUCHEZA

Anasema hana haraka na nafasi yakucheza ndani ya kikosi cha kwanza ambapo kwenye nafasi yake kuna mtu mzima Kapombe, jambo analolifanya ni mazoezi ya nguvu ili akija kupewa kuaminiwa afanye maajabu.

“Wengi wananichukulia kama nimechemka, lakini kwangu naona ni hatua kubwa katika maisha yangu, tayari nimeanza nimeanza kuendana na mazingira ya timu husika na ikumbukwe nimetoka timu ndogo na huu msimu ni wa pili kucheza Ligi Kuu Bara,”anasema.

PRESHA YA MASHABIKI

Anasema amejiunga na timu tajiri ya mashabiki, hivyo anajifunza jinsi yakuishi nao, ili asije akatoka kwenye laini kutokana na wengine kuwa na maneno makali, pindi mchezaji anapokosea.

“Najifunza kujua niishi vipi na hii presha kubwa ya mashabiki kwasababu nimetoka kwenye timu ambayo mchezaji unatakiwa ujipambanie mwenyewe kujipa morali yakutosha ili kufanya vyema, kwa hiyo tofauti kabisa na hapa Simba,”anasema Duchu.

LIPULI IMEMPA MWANGA

Anasema anaamini kucheza kwake Lipuli, kulimpa mwanga wakuonekana na Simba, tofauti na alivyokuwa madaraja ya chini, anakoona hakuzingatiwa kama ilivyo Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Japokuwa nasikitika sana, Lipuli kushuka daraja timu yangu ya kwanza kuichezea ligi kuu, kiukweli naona ndio iliotoa mwanga wa kufika hapa nilipo leo, mpaka mwandishi unajua kuna Duchu,”anasema.

MASTAA WA KIGENI

Anasema Simba ina mastaa wa kigeni, wanaompa akili ya kuwaza mbali hasa akiwaangalia jinsi ambavyo wanaishi na kujituma ili kuwa bora kuliko wengine.

“Huwa najifunza kitu kimoja kwamba kama wao wamekuja nchini kwetu, kumbe hata sisi inawezekana kwenda nchini nyingine na sisi tukawa tunatamba kama wao, najifunza vitu tofauti kutoka kwao,”anasema.

ANGEKUWA MWANAMITINDO

Anasema kama soka lisingetiki basi, angekuwa mwanamitindo kwasababu ndio kazi anayoipenda na mtu anayemtazama kama kioo katika eneo hilo ni beki wa zamani wa zamani wa Manchester United, David Beckham.

“Ni beki ambaye napenda uvaazi wake, licha ya umri wake kumtupa mkono, lakini bado ana mwili ambao akivaa nguo anaonekana yupo smati, hivyo nisingefanikiwa katika soka ningekuwa mwanamindo,”anasema.

VIPI KUHUSU TOTOZ

Anasema kama kuna vitu amevipa kisogo ni mambo ya mapenzi, anaeleza kwamba hana muda nayo na hajawahi kuumizwa, hivyo anapenda kutumia muda wake kupambana ili aweze kubadilisha familia yake kiuchumi.

“Kila jambo lina muda wake, kuhusiana na mapenzi sijui na sina muda nayo, najua nimetoka wapi natakiwa niende wapi, hilo ndilo jambo la msingi, hayo mengine yapo tu na kwanza bado nina umri mdogo sioni haja ya kukimbizana nayo kwa sasa ngoja nitulie,”anasema.