Mhe Msolla naomba nipokelee simu yangu!

Sunday August 2 2020

 

By BADRU KIMWAGA

KAMA upo nje ya nchi, bado naamini wapambe watakufahamisha tu. Lakini kama upo nchini tafadhali mheshimiwa. Naomba unipokelee simu yangu. Kuna jambo nataka kuzungumza nawe. Inawezekana kwa leo ukawa unajiandaa kuichungulia kwa mbali mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC). Ni kweli mechi hiyo inayopigwa alasiri ya kati ya watani zako, Simba na Namungo haikuhusu sana, ila kwa vile wewe ni mtu wa mpira sidhani kama utaikaushia mazima. Hata kama ni kweli kile kipigo cha 4-1 ilichopata timu yako, kilikukata stimu. Achana na ukubwa wa kipigo chenyewe, lakini kule kutibuliwa kwenu njia ya kukata tiketi ya kimataifa, ni wazi bado kimekuvuruga. Lazima kiwavuruge kwa vile wewe na wenzako mmeshindwa kubeba taji lolote tangu muingie madarakani. Nafahamu msimu uliopita mliikutia ligi ukingoni, lakini msimu huu mambo yaliwakalia ovyo. Yaani pamoja na kusajili na kuacha wachezaji kila mlipojisikia, mambo yameenda mrama na watani wenu wametetea taji tena Ligi Kuu!

Sio kutetea tu, lakini pia watani zako wamekulamba 4G na kutibua ndoto za kwenda CAF. Inawezekana ikawepo tena mbeleko, lakini naamini kabisa wanachama na mashabiki wa chama lao hawatakuelewa. Msimu wa pili mfululizo chama lao linashiriki michuano ya CAF kwa HISANI ya Wekundu wa Msimbazi. Wamechoka kejeli na maneno ya Haji Manara. Hawajui ni wapi walibugi hata mambo yamewachachia. Ni misimu michache tu, walikuwa wakiwanyima raha wenzao wa Msimbazi kwa vile chama lao lilitisha kipindi hicho. Waliwanyima raha Simba. Waliwaita Wa Mchangani...Wa Matopeni...Wa Hapahapa kutokana na ukweli kwa miaka karibu sita watani zako walikuwa wakisotea ubingwa. Si unajua taji lao la mwisho lilikuwa lile la 2012 waliokabidhiwa mara baada ya kulichakaza jeshi lako enzi za Wakili Lloyd Nchunga...! Najua huwezi kusahau zile 5-0 za mechi ya Mei 6, 2012.

Najua unaweza kunishangaa imekuwaje nitumie njia hii kukushtua uipokee simu yangu. Nimeona ni bora nitumie njia hii, nikiamini huenda ujumbe huu utakufikia kwa haraka. Maana mheshimiwa umekuwa adimu sana siku hizi. Hata ukipigiwa simu, huna muda wa kuzipokea. Huna mpango wa kujibu maswali yetu tunaotaka ufafanuzi kutoka kwako. Hii ni tofauti na kipindi kile ambacho hakuna aliyekuwa anakufikiria kama ungekuja kuwa kiongozi Jangwani. Kipindi hicho kila lilipojitokeza jambo lililohitajika ufafanuzi wa kina wa kitaalamu. Mheshimiwa ulipopigiwa simu hata kama ingekuwa usiku mwingi, hukuzipuuza simu zetu. Ulizipokea na kutujibia maswali yetu na kutufafanulia kwa upana wengi tukaridhika. Mungu amekujali kipawa cha uchambuzi. Inawezekana ni kwa sababu ya elimu kubwa uliyonayo. Wewe ni kati ya makocha wachache wazawa wenye elimu zao. Labda nisikuchoshe. Lakini nataka tu mheshimiwa uipokee simu yangu, nikueleze tu. Jahazi linazama. Huku mitaani waliokushangilia ulipokuwa ukiingia madarakani, wanakung’onga. Wanadai ni kama kazi imekushinda vile. Kisa ni tabia yako ya kutopenda kujitokeza kutoa ufafanuzi kwa mambo kadhaa tata yanayojitokeza klabuni. Najua sio kila jambo kwa cheo chao hujitokeze kulisemea ama kulitolea ufafanuzi, lakini mambo yanapoenda harijojo, ni lazima hujitokeze kuondoa utata! Ukimya wako unawatisha. Wanashangaa imekuwaje klabu imekuwa na wasemaji wengi, kiasi cha kuwakanganya. Leo anazungumza Hersi Said, kesho anachonga Antonio Nugaz, kesho sijui Hassan Bumbuli na keshokutwa Fredrick Mwakalebela. Ajabu jambo moja, lakini huwa na majibu tofauti. Hii inawachanganya sana. Pia hawajui ule mkataba wa La Liga na mchakato wa mabadiliko ya kuifanya Yanga iendeshwe kisasa umefikia wapi. Ujenzi wa Uwanja wa Kigamboni umeanza ama la...! Pia kuna vurugu za wachezaji nazo zinawachanganya. Juzi kati tena, Kocha Luc Eymael kaamua kuharibu zaidi. Huku mitaani wanachama na mashabiki wa chama lako hawana raha. Watani zao wamepata fimbo ya kuwachapia. Sasa hivi wakionyeshwa ndizi tu, imekuwa ugomvi, lakini Mheshimiwa hujasikika sehemu yoyote kuvunja ukimya kwenye hali tete kama hizi. Jitokeze angalau kutuliza mioyo ya wadau wa klabu yako. Nakumbuka Leodegar Tenga akiwa pale TFF, alikuwa na tabia kama yako za kuwaachia wasaidizi wake wafanye kazi zao. Waseme na kufafanua kila jambo lililo ndani ya uwezo wao. Lakini likitokea jambo zito, alikuwa na desturi ya kuvunja ukimya na kuzungumza. Wadau wa soka wakaridhika na kutuliza mitima yao. Hiki ndicho kilichonisukuma kukuomba unipokee simu, ili kudokeze hili. Kuna wakati lazima uvae viatu vyako ili Wanayanga watulie. Mheshimiwa unajua kama wewe ndiye mhimili wa klabu. Ukimya wako kwa mambo mazito, unawanyima raha wadau wa klabu. Inawezekana ni kutingwa kwako na majukumu ya kazi binafsi ni tatizo. Lakini wanayanga walikuchagua kwa kuamini utawafanyia kazi.

Najua huenda umejiwekea utamaduni tangu uingie madarakani Jangwani, kutopenda kuzungumza, isipokuwa kwenye hafla kubwa kubwa kama zile za Kubwa Kuliko ama usainishwani wa mkataba wa La Liga na Sevilla. Lakini kuna wakati unapaswa kujitokeza kumaliza utata katika mambo yenye utata na yanayowachanganya wadau. Naamini umenipata. Kama hujanipata basi utapata salamu kwa watakaonisoma. Ila muhimu kuipokea simu yangu na za wengine ili utusaidie ufafanuzi huu wa mkataba wa miaka miwili wa BM33. Je ni kweli Papy Tshishimbi anasubiri kuondoka Jangwani? Vipi kuhusu Farouk Shikhalo ni kweli anasepa? Je kuhusu Ramadhani Kabwili michongo yake ipoje? Hawa kina Tuisila na mapro wa kigeni wanaotajwa kila uchao wanatua Jangwani imekaaje? Mchakato wa kumleta kocha wa kuziba nafasi ya Eymael nao umefikia wapi, maana ligi inatarajiwa kuanza. Au haya mambo yote yameachwa kwa mdhamini? Kama ni vivyo mbona hatuwaoni SportPesa aua Afya Water wakiyafanya haya? Pia utusaidie kujua msemaji yupi Jangwani asikilizwe? Ni hayo tu mheshimiwa, ila ukiona ‘missed call’ yangu ujue ninakutafuta nataka tuzungumze! Na ukiiona tena inaita we nipokelee tu, ili unisaidie kunijibia maswali haya yanayoulizwa mitaani!

 

Advertisement