Messi vs Ronaldo : Messi abadili uamuzi, aichezea Argentina

Muktasari:

Hiyo ni habari iliyokuwa gumzo kote Argentina, hakuna aliyepoteza matumaini kwamba mfungaji bora katika historia ya timu ya Taifa ya Argentina atabadili uamuzi na kurudi kwa mara nyingine kuiongoza timu yake ya Taifa.

TOLEO lililopita, mwandishi, Luca Caioli alielezea tukio la Messi kukata tamaa kuichezea timu ya Taifa ya Argentina baada ya kushindwa kuibeba timu hiyo na hatimaye kutangaza kujiuzulu kucheza soka na timu ya Taifa lake. Sasa endelea…

“Hali ndiyo hiyo hilo ni bora kwa kila mmoja wetu, hatuwezi kuridhika kwa kufikia fainali na tusiwe washindi, nimepambana kwa wakati wangu na kujaribu mara nyingi ili niwe bingwa na Argentina haikuwezekana, sitoweza kufanya hivyo.

Baada ya kushindwa fainali nne (mwaka 2007, 2015 na 2016 Copa America na Kombe la Dunia 2014), Lionel ni kama alijikatia tamaa, aliamua kukubali yaishe, na kustaafu kuichezea timu ya Taifa ya Argentina.

“Sote tulifanyiziwa na mtu ambaye alifanyiziwa zaidi zaidi ni Messi, huo ni upande mbovu zaidi niliowahi kuuona kwenye vyumba vya kubadilishia nguo,’’ anasema straika wa Man City Kun Aguero kupitia mtandao wa kijamii kuhusu habari iliyozagaa mitandaoni yenye kauli mbiu ‘Messi usiondoke.”

Hiyo ni habari iliyokuwa gumzo kote Argentina, hakuna aliyepoteza matumaini kwamba mfungaji bora katika historia ya timu ya Taifa ya Argentina atabadili uamuzi na kurudi kwa mara nyingine kuiongoza timu yake ya Taifa.

Na Agosti 12, 2016 matumaini hayo yalitolewa baada ya Messi kuthibitisha katika mkutano na waandishi wa habari kwamba alikuwa akifikiria kuendelea kucheza soka la kimataifa akiwa na timu yake ya Taifa, na hivyo kubadili wazo lake la awali la kuachana na timu hiyo.

“Naipenda nchi yangu, na naipenda sana jezi ya timu ya Taifa, naona kuna tatizo na soka la Argentina sitaki kutengeneza tatizo jingine, namshukuru kila mmoja ambaye anataka mimi niendelee kuichezea Argentina na natumaini tutawapa raha si muda mrefu,’’ alimaliza kwa kusema Messi.

Maisha ya Messi pengine yanahitaji kuwa na aina ya vituko vyake amekuwa ni mtu wa kupata mafanikio na ana changamoto zake na labda changamoto kubwa ni kuwasili kwake Hispania miaka hiyo iliyopita.

Alifika Barcelona akiwa na baba yake Septemba 17, 2000, tayari alikuwa ameshafahamika katika soka huko Argentina ambako gazeti moja lilitoa kurasa mbili kuelezea mafanikio yake.

Na sasa amefika Barcelona makao makuu ya Catalan kuonyesha kwamba kila kile kilichokuwa kikisemwa kumhusu yeye kina ukweli na ni wazi kwamba alimvutia kila mtu wakati wa majaribio.

“Nilikuwa natoka kwenye chakula na moja kwa moja nikaingia uwanjani dakika tano baadaye, timu mbili tayari zilishaanza kucheza, anakumbuka Carles Rexach ambaye kwa wakati huo alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Barcelona.

“Nililazimika kukimbia kupitia uwanjani ili nifike kwenye benchi ambako kulikuwa na makocha, ilinichukua dakika saba au nane kujua kila kitu.

“Wakati nikiwa nimekaa kwenye benchi nilikuwa nimeshafanya uamuzi wangu, niliwaambia Rife na Migueli (makocha wa timu ya vijana) ‘Tunahitaji kumsajili sasa’.

“Nini hiki nimeona, mtoto ambaye alikuwa na umbo dogo lakini yuko tofauti ana hali ya kujiamini ya ajabu mwepesi, makini ana kasi na mwenye uwezo wa kumhadaa yeyote atakayejitokeza mbele yake, haikuwa vigumu kuyaona hayo, kuona kipaji chake ambacho kwa sasa kimejulikana kwa kila mtu, kimeonekana zaidi akiwa na miaka 13.

“Kuna wachezaji wanaohitaji timu ili wang’are lakini si yeye, kwa wote ambao wananiambia mimi kwamba ndiye niliyemvumbua Messi wakati wote huwa nawajibu, hata watu wanaoishi katika sayari nyingine wakimuona watakubali kwamba ni mtu wa kipekee.”

Itaendelea Jumamosi ijayo